Sunday, May 13, 2018

Ubingwa Yanga ulikwama hapa

Tags

INGAWA mashabiki wa Yanga bado hawaamini kuwa timu yao imetemeshwa taji la ubingwa wa Ligi Kuu Bara, na kutua mikononi mwa mahasimu wao, Simba. Wekundu wa Msimbazi, walitwaa taji hilo Alhamisi iliyopita baada ya Yanga kupokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Tanzania Prisons ya Mbeya na kuifanya Simba kutawazwa mabingwa wakiwa nje ya uwanja tena hotelini wakielekea mjini Singida.
Simba imechukua taji hilo kutoka kwa Yanga ambao ndiyo waliokuwa wakilishikilia kwa misimu mitatu mfululizo, lakini msimu huu mambo yakabadilika sana kwao.
Yanga imepoteza mataji yote msimu huu ukiwa ni msimu wa hasara zaidi, ikibaki na heshima moja tu itakayotamba nayo kwa kufuzu hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kupoteza kwao mataji kwa michuano yote ya msimu huu, ina maana haitashiriki michuano ya kimataifa ikiwa ni mara ya kwanza tangu 2012. Yote kwa yote, kuna sababu nyingi ambazo zimeinyima Yanga ubingwa msimu huu, Mwanaspoti inaangazia sababu tano za msingi.
KIKOSI DHAIFU
Baada ya kutesa kwa misimu minne mfulizo kwa kuwa na kikosi chenye ubora mkubwa, msimu huu Yanga ilianguka na sababu kubwa ni kuwa na kikosi chembamba kilichokosa ubora. Yanga ya msimu huu haikuwa na afya. Haikukamilika na walianza msimu wakionekana wachovu huku wachezaji wengi vijana waliokosa ujasiri wa kuipa mafanikio timu hiyo.
Ikumbukwe kuwa Yanga hawakufanya usajili mkubwa kama ilivyozoeleka, ukiondoa Obrey Chirwa, Papy Kabamba Tshishimbi na mabeki Hassan Kessy, Gadiel Michael, Kelvin Yondani na Andrew Vincent ‘Dante’ walioonekana kuwa wapambani wa kweli huku wengine wakionekana wa kawaida.
MAJERUHI WASIOPONA
Ndani ya kikosi hicho dhaifu likaibuka janga jingine ambalo ni lundo la majeruhi. Tena kibaya zaidi ni kwamba, majeruhi hao walianza hata kabla ya ligi na baada ya ligi kuanza na mpaka msimu unamalizika hawakuweza kupona.
Hebu piga hesabu, Yanga ilianza msimu na matumaini yao yakiwa kwa wachezaji wakongwe kiungo Thabani Kamusoko, washambuliaji Amissi Tambwe na Donald Ngoma. Wakati wakiwa na matumaini hayo wakongwe hao wote hawajaweza kucheza hata robo msimu.
UONGOZI MBOVU
Tangu kuondoka kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji uongozi wa timu hiyo uliyumba kabisa. Yanga imekuwa chini Kaimu Mwenyekiti, Clement Sanga ambaye viatu vya Manji vimekuwa vikubwa kwake. Kibaya zaidi likaibuka anguko la ubovu wa sekretarieti yake. Muundo wa uongozi wa klabu, siku zote timu husimamiwa na Sekretarieti, lakini ikiwa chini ya Charles Mkwasa haikuweza kuwa afya ya kuisimamia vyema timu.
Mambo yaliyumba na mpaka sasa yanayumba na kuonyesha wazi kwamba, kuna tatizo ndani ama wanakosekana watu sahihi wa kuiongoza Yanga na kuitoa kwenye kipindi kigumu.
MANJI NA NOTI ZAKE
Kikosi cha Yanga hakijawahi kuwa na maisha mazuri kwa miezi miwili mfululizo msimu huu. Kwa maana ya wachezaji na watendaji wengine kulipwa mishahara yao kwa wakati. Yanga ilikuwa na udhamini lakini bado mambo yalizidi kuonekana magumu. Tatizo ni kwamba nakisi ya fedha hasa mchango aliokuwa anautoa Manji ndani ya klabu hiyo ilionekana hata alivyoondoka hakuna aliyekuja kuziba nafasi yake.
Klabu iliyumba na kibaya zaidi timu hiyo imerudi katika maisha yao ya nyuma kwa kusafiri na basi kuelekea Mbeya na timu kufika saa sita usiku na kesho yake wakashuka uwanjani kucheza na Prisons ya Mbeya na kuchukua kipigo cha mabao 2-0.
Ndani ya Yanga hali ya migomo kwa wachezaji ilikuwa ni kitu cha kawaida na kufikia hatua hata aliyekuwa Kocha Mkuu, George Lwandamina kulazimika kukimbia hali hiyo ngumu ya fedha akirudi zake Zesco ya Zambia.
SIMBA NA MO WAO
Habari mbaya zaidi kwa Yanga msimu huu ni kuibuka kwa Simba ambayo ilijivua gamba kwa kuondokana na maisha yao ya kubahatisha waliyoishi kwa miaka mitano iliyopita na kuamua kufanya kweli msimu huu.
Simba msimu huu walisajili kikosi kizito kilichoundwa na wachezaji wanaojua kujiongeza na walionyesha wanataka mafanikio. Kikosi hicho kinatajwa kuwa na thamani ya Sh1 bilioni.
Maisha yao ya kulialia njaa yalifikia tamati baada ya kurejea kwa Bilionea wao, Mohammed Dewji ‘MO’ ambaye alisajili timu hiyo na kuigharamia karibu kila kitu na gharama hizo kulipa kwa kurejea kwa ubingwa.
WASOMI WAFUNGUKA
Wakitoa mitazamo yao kulingana na anguko hilo la Yanga aliyekuwa Katibu Mkuu wa Yanga, Dk. Jonas Tiboroha alisema kuporomoka kwa Yanga kumetokana na uongozi kushindwa kusoma alama za nyakati.
Amesema Yanga ilitakiwa kujiendesha yenyewe, lakini tatizo likawa uongozi ambao ulishindwa kuwa na mipango ya muda mfupi na muda mrefu huku wakiishi maisha ya zima moto.
“Matatizo ya Yanga ni uongozi kushindwa kusoma alama za nyakati na mambo yanaendeshwa kienyeji sana. Hakukuwa na mpango mkakati wa muda mfupi wala mrefu. Ukata klabuni ulikuwa mkubwa kupitiliza. Wachezaji hawakuwa na furaha na kibaya zaidi wachezaji wao muhimu walikosekana kwa muda mrefu,” alisema Tiboroha.
“Yanga imepoteza muelekeo na kukosa ubingwa kwa matatizo ya nje ya uwanja kwa kiasi kikubwa, lakini kibaya zaidi sioni jitihada za uongozi kuondoa hiyo hali. Hawakuweza kuwaunganisha wanachama na mashabiki, lakini kibaya zaidi hawakuwa na jitihada za kutatua matatizo ya kiuchumi na kuiondoa timu katika hali mbaya kifedha.”
Mbali na Tiboroha mwingine aliyetoa mtazamo wake ni Dk. Mshindo Msolla akisema anguko la Yanga limetokana na mambo matatu makubwa ambayo ni kukumbwa na hali ngumu ya kiuchumi, kufanya usajili mbovu na kushindwa kutumia mtaji wa wingi wa wanachama.
“Tangu Manji apate matatizo klabu iliyumba kiuchumi, uongozi haukuwa na njia mbadala kwa kuwa walishategemea nguvu ya mtu mmoja, lakini usajili wao haukufanyika vizuri. Walisajili wachezaji wengi ambao umri wao ulikuwa mkubwa,” alisema Msolla ambaye kitaaluma ni kocha.
“Wachezaji waliotegemewa hawakuwa na tija kwenye timu, lakini kibaya zaidi lilipokuja dirisha dogo la usajili ambalo walitakiwa kujisahihisha wakakumbana na ukata na kushindwa kusajili lingine ni tatizo la benchi lao la ufundi.
“Benchi la ufundi halikujua aina ya wachezaji waliokuwepo kikosini. Kocha aliyepita (Lwandamina) alipaswa kujua matatizo ya wachezaji wa Kitanzania, lakini aliwafundisha kama vile wachezaji wa Zambia ambao wanajitambua kibaya tena hata wasaidizi wake hawakuwa na msaada mkubwa kwake. Lwandamina aliamini anafanya kazi na wachezaji wanaojielewa na kufuata misingi ya wachezaji wa kulipwa, lakini mambo ni tofauti kabisa kwa soka letu,” alisema.
Credit: Mwanaspoti