Tishio Jipya Penzi La Mobeto Na Mond Hili Hapa!


HILI ni tishio jipya! Ndivyo unavyoweza kusema kwani ukiachana na kipigo ambacho mama wa mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Sanura Kassim ‘Sandra’ alimshushia mwanamitindo Hamisa Mobeto hivi karibuni, tishio jipya limeibuka.
Tishio hilo ni la msanii Suzan Michael ‘Pretty Kind’ kuibuka na kudai kuwa, atapambana vilivyo kuhakikisha anamng’oa Diamond kwa Mobeto.
Kwa nini ni tishio?
Pretty, msanii wa muziki na filamu mwenye shepu matata, macho yanayoita na sauti nyororo anakuwa tishio kwenye penzi la Mobeto kufuatia maelezo yake kwamba, kwa muda mrefu amekuwa akimuwinda Diamond hivyo anaona ni wakati muafaka wa kuchukua nafasi.
“Nitamng’oa tu Diamond kwa Mobeto kwa sababu nampenda sana, ananikosesha usingizi, huyo Mobeto asidhani amefika. “Wakati f’lani niliona ni ngumu kumpata Diamond kwa kuwa mama yake alikuwa akimpenda sana Mobeto lakini sasa hivi naona njia nyeupe baada ya Mobeto kuchezea kichapo,” alisema Pretty.
Pretty ambaye hivi karibuni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza, alimfungia kujihusisha na sanaa kufuatia skendo yake ya kupiga picha chafu (baadaye alifunguliwa), aliyanena hayo alipokuwa akifanyiwa mahojiano na gazeti hili hivi karibuni. Fuatilia hapa chini…
Risasi Jumatano: Unadai unampenda sana Diamond na utamng’oa kwa gharama yoyote kwa Mobeto, unadhani utafanyaje wakati wengine wameshindwa?
Pretty: Hahaaa! Swali lako linanifanya nicheke kwa sababu hunijui vizuri, nitamng’oa tu na mtashangaa. Hao walioshindwa ni wao, mimi nitaweza tu, nina mikakati kabambe kwani nikiamua langu, lazima liwe. Wanaonijua wananielewa. Waulize wasichana niliokuwa nao India.
Risasi Jumatano: Mwenzako ameshajihakikishia penzi, wewe unataka kumletea shobo, huogopi?
Pretty: Hata simuogopi huyo Mobeto, angekuwa ameolewa sawa lakini hajaolewa na wala Diamond hajawahi kutangaza mpenzi au mchumba wake kwa sasa. Mimi nasema, wasionijua watanijua.
Risasi Jumatano: Lakini wamezaa, si rahisi kuwaachanisha kirahisi, utafanyaje?
Pretty: Zari kazaa watoto wawili, mahaba yalikuwa motomoto na wameachana sembuse yeye mwenye mtoto mmoja, atashangaa, hata mimi nina kizazi.
Risasi Jumatano: Au utatumia ndumba kama ulizokuwa ukitumia India za kuwanasa wanaume?
Pretty: Nilishasema situmii ndumba ila mimi ni mwanamke, najiamini na hakika nitamnasa kwa njia ambayo wote mtashangaa.
Risasi Jumatano: Kwa nini umeamua kumnasa Diamond na si mwingine?
Pretty: Nimejikuta tu navutiwa naye na kwa ninavyoona hata yeye ananipenda kwani tunaendana kiaina.
Risasi Jumatano: Mnaendana kiaina! Ina maana mlishakutana? Au wewe umejuaje kama mnaendana?
Pretty: Usitake kuchunguza, sisi wote ni wasanii, siyo lazima ujue kinachoendelea.
Mbali na majigambo hayo ya Pretty ya kutaka ‘kukitia mchanga kitumbua’ cha mwenzake, wapo wengine ambao wanaomba usiku na mchana Diamond asimuoe Mobeto huku ‘wagawa ubuyu’ wakianika kuwa, Pretty amekuwa akijilengesha sana kwa Diamond na kwa kasi aliyo nayo huenda akafanikiwa.
Ndoto za Mobeto zazidi kufifia
Tangu Zari aamue kumwaga manyanga, Mobeto amekuwa akijiaminisha kwamba yeye ndiye wa kuolewa na Diamond lakini yametokea mazengwe kadha wa kadha ambayo yanaifanya ndoto yake ififie.
Zari mara kadhaa amekuwa akitoa maneno ya laana kwa Mobeto akionesha kuwa, yeye ndiye aliyevuruga penzi lake hivyo naye amekuwa akimuombea yamfike. Mama Diamond naye licha ya juzikati kumpa kipigo Mobeto, amekuwa akiweka wazi kuwa, hayuko tayari kuona Diamond anamuoa mwanamama huyo.
Naye baba wa Diamond, Abdul Juma akizungumza na gazeti hili hivi karibuni licha ya kutokubaliana na kitendo cha mama Diamond kumpiga Mobeto, naye alionesha kutompenda mwanamitindo huyo hasa kufuatia kumpotezea baada ya penzi lake na Diamond kunoga.
Diamond, Mobeto wanasemaje?
Gazeti hili lilifanya jitihada za kumtafuta Diamond kupitia simu yake ya mkononi ili kujua kama anayo nafasi kwa Pretty lakini jitihada ziligonga mwamba baada ya simu yake kuita bila kupokelewa.
Naye Mobeto alipopigiwa simu hakupokea na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno ‘sms’ akitakiwa azungumzie tishio hilo jipya kwenye penzi lake hakujibu. Hata hivyo, maneno ambayo Mobeto amekuwa akiyaposti kupitia ukurasa wake wa Instagram yamekuwa yakionesha kuwa, kwa Diamond amefika na hakuna anayeweza kumng’oa
MaoniMaoni Yako