Simba yataka kunogesha ubingwa Singida

  • ***Yapania kushinda leo kuendeleza rekodi ya kutofungwa mpaka sasa....
MABINGWA wapya wa ligi kuu Tanzania Bara, Simba, leo wanashuka kwenye uwanja wa Namfua mjiniS ingida kucheza na wenyeji wao, Singida United huku kocha wao msaidizi Masoud Djuma, akisema wanataka kunogesha ubingwa wao kwa ushindi.

Mbali na kutaka kunogesha ubingwa wao kwa ushindi leo, pia wanataka kuendeleza rekodi yao ya kucheza msimu huu bila kupoteza mchezo wowote.
Mpaka wanajihakikishia ubingwa, Simba imecheza michezo 27 , imeshinda michezo 19 na kutoka sare michezo 8 na haijafungwa mchezo wowote huku ikikusanya pointi 65 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote hata kama watapoteza michezo yote mitatu iliyobakia.
Katika michezo hiyo pia imeweka rekodi ya kufunga mabao 60 huku nyavu zake zikitikiswa mara 13 tu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Djuma, alisema ingawa tayari wametwaa ubingwa, wanataka kuhakikisha wanamaliza michezo yao mitatu iliyobakia bila kupoteza mchezo wowote.
"Hatutaki kuweka doa kwenye sherehe za ubingwa wetu, mchezo hautakuwa mwepesi kwa sababu Singida tuliwafunga mchezo wa kwanza na najua watataka kulipiza kisasi lakini tumejiandaa kukabiliana nao," alisema Djuma.
Alisema kuwa hawataudharau mchezo wa leo kwa kuwa tayari wameshatwaa ubingwa na watapambana kama ilivyokuwa kwenye michezo iliyopita.
"Wachezaji wana molali ya juu, tunaingia uwanjani kusaka pointi tatu ili kuendeleza rekodi yetu ya kutopoteza, hatutapunguza kasi yetu," alisema.
Kwa upande wake, kocha wa Singida United, Hans van der Pluijm, alisema wanaiheshimu Simba kwa mafanikio yao msimu huu lakini hawatakubali kupoteza mchezo wa leo.
Baada ya mchezo wa leo, Simba itarejea Dar es Salaam kujiandaa kuvaana na Kagera Sugar kabla ya kuelekea Songea kuhitimisha msimu huu wa ligi kuu kwa kuvaana na Majimaji ya mjini humo.
Credit: IPP Media