Simba, Yanga zanukia kucheza na Everton England


Bingwa wa michuano ya Super Cup ya mwaka huu, itakayoshirikisha vilabu nane, nne kutoka Kenya na nne kutoka Tanzania ataenda Goodison Park kukutana na Everton FC.
Akizungumza katika uwanja wa Kasarani, jijini Nairobi, kabla ya kuanza kwa mechi ya kirafiki ya Hull City Challenge, kati ya mabingwa wa soka nchini, Gor Mahia na Hull City, inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini Uingereza, Mkurugenzi wa SportPesa, Captain Ronald Karauri alisema michuano hiyo itafanyika Juni, mwaka huu.
Mashindano hayo huhusishwa timu ambazo zinadhaminiwa na SportPesa ambapo Simba, Yanga na Singida United zinadhaminiwa kwa hapa nchini.
Akionesha kuridhika na idadi kubwa ya mashabiki waliofurika katika uwanja huo, Karauri alisema mwaka huu, Everton hawatosafiri kuja Afrika, na badala yake, mabingwa wa Super Cup, watakweya pipa hadi Goodson Park kuwakabili Everton.
"Nimevutiwa sana na muitikio wa mashabiki, sikutegemea uwanja wa Kasarani kufurika kiasi hiki, kutokana na hiki mlichokifanya, bingwa wa Super Cup, ataenda England kukutana na Everton," alisema Karauri.
Mwaka Jana, Gor Mahia walipata nafasi ya kupimana ubavu na Everton Jijini Dar es salaam, baada ya kutwaa uchampioni wa Super Cup 2017.
 Credit: Mwanaspoti