Monday, May 21, 2018

Simba yamzawadia taji Mafisango

Tags

JUZI kati, yaani Alhamisi tu iliyopita mashabiki wa Simba walikuwa wakiadhimisha mwaka wa sita tangu aliyekuwa nyota wao, Patrick Mafisango, alipoaga dunia kwenye ajali ya gari Mei 17, 2017.
Mashabiki wa Simba hawamsahau kiungo huyo fundi aliyekuwa katika kikosi kilichokuwa kimebeba taji la mwisho kabla ya mwaka huu Wekundu wa Msimbazi kukata minyonyoro ya ukame kwa kubeba taji walilokabidhiwa jana Jumamosi.
Lakini kumbe sio mashabiki tu wa Simba, hata mastaa wa klabu hiyo wanaendelea kumkumbuka Petit a.k.a Papaa Mafisango.
Winga, Shiza Kichuya alisema hajamsahau Mafisango katika mafanikio ya ubingwa, waliyoyapata msimu huu.
Japo Kichuya hakuwa katika kikosi cha mwisho kilichobeba ubingwa msimu wa 2011-2012, lakini alisema Mafisango na Haruna Moshi ‘Boban’ ni wachezaji waliochangia mafanikio yake kutokana na kuwafuatilia na kupenda soka lao.
Kichuya alisema Mafisango anakumbukwa na nyota wa Simba na hasa kila wanapoona mashabiki wakitimba uwanjani na bango lenye jina na sura ya kiungo huyo Mnyarwanda aliyekuwa na asili ya DR Congo.
“Sikucheza pamoja naye, lakini kwa namna alivyokuwa anaupiga mwingi ndio sababu ilikuwa inafanya nikimbilie katika bango lake kabla ya ubingwa,” alisema.
Naye Shomary Kapombe aliyecheza na Mafisango, alisema ubingwa walioupata, umemkumbusha mbali jinsi staa huyo raia wa Congo, alivyokuwa mshauri wa wenzake kuamini katika kufanikiwa.
“Mechi yake ya mwisho ilikuwa na Yanga ambayo tuwaliwafunga mabao 5-0, Mafisango alikuwa kati ya wachezaji mwiba kwa siku hiyo.
“Hivyo ubingwa huo umenifanya nitamani angekuwepo, naamini angekuwa na furaha ya ajabu, hata hivyo tuliokuwepo yaani Emmanuel Okwi, Jonas Mkude na Mwinyi Kazimoto, tumemwakilisha vema,” alisema.
Naye kiungo Said Ndemla alisema licha ya kwamba alikuwa kikosi B wakati huo, lakini alikuwa anamfuatilia Mafisango.
“Nilikuwa ndio nachipukia na kutamani kuwa kama yeye, ubingwa huu ni heshima kwake,” alisema.
Credit: Mwanaspoti