Simba mwendo wa rekodi 2009/10

  • ***Kapombe ailiza Singida, sasa wabakia Kagera Sugar na Majimaji ...
USHINDI wa bao 1-0, iliyoupata Simba dhidi ya Singida United kwenye Uwanja wa Namfua jana, umeiweka timu hiyo ya mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam katika nafasi nzuri ya kurejea rekodi yake ya msimu wa 2009/10.

Msimu wa 2009/10, Simba ilitwaa ubingwa bila kupoteza mechi yoyote, hivyo wakati huu ikikabiliwa na michezo miwili iliyobaki dhidi ya Kagera Sugar ya Kagera na Majimaji FC ya Songea, inahitaji sare yoyote  ama ushindi ili kufikia rekodi hiyo.
Hadi sasa Simba ambayo jana imefikisha pointi 68, haijapoteza mechi yoyote kati ya 28 ilizocheza, huku ikishinda 20 na kutoka sare nane.
Aidha, Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, tayari ndiyo Bingwa katika msimu huu wa 2017/18, hivyo inachokitafuta kwa sasa ni kushinda tu ama kutoka sare ili kuweka rekodi ya kutokupoteza msimu huu.
Katika mechi hiyo ya jana ambayo ilichezeshwa na mwamuzi, Shomary Lawi kutoka Kigoma, Simba ndiyo ilipata bao hilo pekee katika dakika ya 24 kupitia kwa Shomary Kapombe baada ya kipa  Ally Mustapha "kutema" shuti la John Bocco na kurudi kujaa mguu wa kulia wa Kapombe aliyeuzamisha kimyani.
Hata hivyo, Singida ambayo nayo inadhaminiwa na SportPesa, ilishambulia ikitaka kusawazisha lakini ilipoteza nafasi kadhaa kupitia kwa wachezaji wake, Kambale Salita, Deus Kaseke na Danny Usengimana ambaye aliingia akitokea benchi.
Katika mchezo huo ambao kocha wa Simba, Pierre Lechantre, alikuwa na mipango ya kushambulia zaidi akiwaanzisha  washambuliaji watatu, Bocco, Emmanuel Okwi na Laudit Mavugo, mipango yao ilionekana kukwama kutokana na uimara wa beki ya Singida.
Simba ilifanya mabadiliko dakika ya 51 kwa kumtoa Mavugo na kumuingiza Haruna Niyonzima, huku Singida ikimtoa Kambale na kumuingiza Danny Usengimana dakika ya 56, pia Elinywesia Sumbi akichukua nafasi ya Salum Chuku dakika ya 63.
Kwa Matokeo hayo, Singida inayonolewa na Mholanzi Hans van der Pluijm inabaki nafasi ya tano na pointi zake 41.

KABLA YA MECHI
Mashabiki walianza kuingia uwanjani tangu asubuhi na ilipofika majira ya saa nne uwanja ulishatapika isipokuwa eneo la Jukwaa Kuu.
Singida United ilikuwa ya kwanza kuingia uwanjani majira ya saa 9:09 alasiri huku Simba ikingia saa 9:20.
Wachezaji wa Simba waligawa jezi za mazoezi kwa mashabiki baada ya kupasha huku Kocha Lachantre yake akimzawadia mtoto mdogo wa takriban miaka minne Isaka Jonas.
Chanzo: IPP Media