Simba heshima leo, Yanga jasho, damu

  • ***Vita vya nafasi ya pili na kushuka daraja Ligi Kuu ikifikia ukingoni...
PAZIA la Ligi Kuu Tanzania Bara linafungwa rasmi leo kwa timu zote 16 kushuka uwanjani kukamilisha mechi zao za mwisho.

Ingawa Simba tayari imeshatangazwa bingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2017/18, leo itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea ikisaka heshima dhidi ya Majimaji wakati huu ikiwania kushinda ili iwe imemaliza ligi hiyo kwa kupoteza mechi moja tu.
Hata hivyo, utamu wa mwisho unabaki katika kufahamu timu gani itamaliza ligi katika nafasi ya pili nyuma ya Simba.
Mbio za nafasi hiyo zipo kwa Azam na Yanga ambazo zinacheza leo usiku kwenye Uwanja wa Taifa.Kila timu ina nafasi ya kumaliza nyuma ya Simba kama itashinda mchezo huo.
Sare ya bao 2-2 dhidi ya Ruvu Shooting ndiyo iliyoiweka Yanga kwenye nafasi ngumu zaidi kumaliza nafasi ya pili kabla ya mchezo wa leo.
Azam inaizidi Yanga kwa pointi mbili tu, hivyo endapo 'Wanajangwani' hao watashinda mechi ya leo, watafikisha pointi 55 sawa na 'Wanalambalamba' hao.
Hata hivyo, Yanga ina tofauti kubwa ya mabao ya kufunga na kufungwa, hivyo endapo itashinda ni wazi itamaliza ya pili, lakini Azam yenyewe inahitaji sare tu ili kujihakikishia nafasi hiyo.
Nahodha wa Azam, Himid Mao, ameweka wazi kuwa wanaitaka nafasi ya pili.
"Ushindi ndio jambo pekee tunalolitaka, tunataka nafasi ya pili, lakini pia tunataka kulipiza kisasi cha kufungwa kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza, " alisema Himid.
Lakini pia, beki na nahodha msaidizi wa Yanga, Kelvin Yondani, alisema wanataka kumaliza kwa ushindi msimu huu.
VITA YA KUSHUKA DARAJA
Mbali na kusubiria kuona nani anakuwa nyuma ya Simba, kwa upande wa pili kuna uhondo upo kwenye kufahamu timu gani itaifuata Njombe mji kwenye kushuka daraja msimu huu.
Tayari Njombe Mji imeshajihakikishia kurudi ilipotoka na kuacha vita kati ya Ndanda FC na Majimaji ambazo mojawapo itashuka daraja kutegemeana na matokeo watakayoyapata leo.
Majimaji ambayo itakuwa mwenyeji wa Simba, matokeo yoyote mbali na ushindi huku Ndanda ikishinda dhidi ya Mwadui kwenye mchezo wao, itawafanya 'Wanalizombe' hao wa Songea kuungana na Njombe kushuka daraja.
Mechi zingine za kukamilisha ratiba hiyo zitakazopigwa leo ni pamoja na Lipuli FC ambayo itakuwa mwenyeji wa Kagera Sugar, wakati Tanzania Prisons ikiialika Singida United.
Mtibwa Sugar itakuwa mwenyeji wa Mbeya City huku Mbao FC ikiialika Ruvu Shooting na vibonde wanaorejea Ligi Daraja la Kwanza, Njombe Mji wakiwa wenyeji wa Mwadui FC. 
Credit: IPP Media
MaoniMaoni Yako