Simba hesabu kwa Singida Utd

BAADA ya kufanikiwa kupata ushindi kwenye mchezo dhidi ya watani zao Yanga, vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, sasa imeanza kuiwekea mikakati Singida United.
Simba itaanza kucheza na Ndanda FC Mei 6, kwenye Uwanja wa Taifa kabla ya kwenda Singida kuivaa Singida United katika
Uwanja wa Namfua, Mei 13, mwaka huu na endapo itafanikiwa kupata ushindi kwenye michezo hiyo, rasmi itatawazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu msimu huu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha msaidizi wa timu hiyo, Masoud Djuma, alisema mchezo dhidi ya Singida United nao ni mgumu kutokana na uimara wa timu hiyo na tayari wameanza mikakati ya kuhakikisha wanapata ushindi.
"Tuliwafunga hapa Dar es Salaam mabao manne, lakini hiyo haimaanishi wana timu mbovu au tutapata ushindi kirahisi, tunajua mchezo utakuwa mgumu na ndio maana tunajiandaa dhidi yao na hata Ndanda FC ambao tutaanza kucheza nao hapa," alisema Djuma.
Alisema, lakini pia wanautazama kwa jicho la pili mchezo dhidi ya Ndanda FC utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa.
Kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa kama ilivyo kwa Yanga na Singida United, iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Simba ambayo iliilaza Yanga bao 1-0 Jumapili iliyopita na kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa msimu huu, inahitaji ushindi kwenye michezo miwili tu kati ya minne iliyobakia ili kutwaa ubingwa.
 Chanzo: Championi