Serikali: Sababu kumbariki Mo Simba


  • ***Apongezwa huku wanachama wakiridhia mabadiliko hayo na sasa...  
MCHAKATO wa Klabu ya Simba wa kufanya mabadiliko ya uendeshwaji umeiva baada ya serikali  kubariki na kuruhusu kuendelea, ambapo sasa mfanyabiashara Mohamed 'Mo' Dewji atamiliki hisa asilimia 49 huku 51 zikibaki kwa wanachama.
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Harrison Mwakyembe, amesema wamebariki mabadiliko hayo ya Katiba ya Simba ambayo yanaenda kuupokea rasmi mfumo mpya na wa kisasa wa uendeshwaji wa klabu hiyo kwa sababu haukwepeki kwa sasa.
Mwakyembe ameeleza hayo punde kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, ambapo Simba walifanya mkutano mkuu wa dharura kwa ajili ya maboresho ya katiba yao.
Waziri huyo amesema ni wakati mwafaka sasa kwa klabu za Tanzania kuingia katika mfumo huo ambao umejikita kibiashara na wenye mafanikio makubwa huku akieleza kuwa haukwepeki.
Aidha, Mwakyembe amempongeza Mo Dewji, kwa kuamua kuwekeza ndani ya Simba akiamini ataibadilisha zaidi klabu hiyo kuweza kufika mbali kimataifa.
"Ni matarajio yetu mfumo huu utaipa mafanikio klabu ya Simba kuweza kufanya vizuri kimataifa, nampongeza Dewji kwa uamuzi wake huu.
Alisema, serikali imeruhusu rasmi mabadiliko hayo hasa baada ya kupata mwekezaji anayewekeza asilimia 49 kama ambavyo taratibu zinavyotaka.
Katika hatua nyingine, uongozi wa klabu ya Simba kupitia kwa makamu wake wa Rais, Salim Abdallah 'Try Again' umemkabidhi zawadi ya jezi yenye namba 19 Rais, Dk. John Magufuli.
Rais Magufuli juzi aliikabidhi Simba kombe la ubingwa baada ya mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar ambao walikumbana na kipigo cha bao 1-0.
Makamu huyo wa Rais, alisema zawadi hiyo kwa Rais Magufuli ilipaswa kutolewa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, lakini kutokana na ufinyu wa ratiba walishindwa kutimiza lengo hilo.
Jezi hiyo ilikabidhiwa kwa waziri Mwakyembe huku ikiwa imeandikwa JPM 19, kuashiria mataji 19 waliyoyatwaa kwenye Ligi Kuu tangu kuanzishwa kwake.
Credit: IPP Media
MaoniMaoni Yako