Serengeti Boys: Ubingwa Cecafa haukuwa rahisi

NYOTA wa timu ya Vijana ya Taifa ya umri wa chini ya miaka 17 ya Tanzania (Serengeti Boys), Edson Jeremiah, amesema haikuwa kazi rahisi mpaka kufanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya Afrika Mashariki na Kati inayoandaliwa na Baraza la Soka la Ukanda huo (CECAFA).

Kikosi cha Serengeti Boys kiliwasili nchini alfajiri ya kuamkia jana na kupokelewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe.
Akizungumzia ubingwa huo walioupata baada ya kuifunga Somalia mabao 2-0 kwenye mchezo wa fainali, nyota huyo wa Serengeti Boys, Jeremiah, alisema michuano hiyo haikuwa rahisi.
"Mashindano yalikuwa magumu na ilitupasa kupambana, kila timu ilikuwa imejianda na ilitoa ushindani mkubwa, tunashukuru tumefanikiwa kutwaa ubingwa," alisema Jeremiah.
Alisema siri ya kufanikiwa kwao ni kujituma pamoja na kufuata maelekezo ya kocha wao.
Kikosi cha timu hiyo kinajiandaa kushiriki kwenye michuano ya Afrika ya vijana ambayo itafanyika hapa nchini mwakani.
IPP Media
MaoniMaoni Yako