Sahau Okwi, Bocco hawa wameibeba Simba


Dar es Salaam. Simba imefunga mabao 60, hadi sasa huku washambuliaji wake pacha John Bocco na Mganda Emmanuel Okwi wakiwa wamefunga magoli 34, na wachezaji wengine tisa wakizifumania nyavu mara 26.
Mwanaspoti Online inakuleta mastaa waliochangia mabao 26 nje na yale yaliyofungwa na Okwi 20 na John Bocco 14.
Katika safari ya kusaka ubingwa wa Simba msimu huu, huwezi kuacha kuwataja winga Shiza Kichuya anayeshika nafasi ya tatu kwa kufunga mabao saba kabla ya kubadili majukumu yake na kuwa mtoaji wa pasi za mabao kwa Okwi na Bocco.
Mbali ya Kichuya wengine waliofunga mabao mengi ni beki Asante Kwasi tangu amejiunga na timu hiyo amefanikiwa kufunga mabao matatu (3) na mechi yake ya mwisho kufunga ilikuwa dhidi ya Mbeya City.
Kiungo Mzamiru Yassin pamoja na kuwa na wakati mgumu wa kupata namba tangu ujio wa Mfaransa Pierre Lechantre amefanikiwa kufunga mabao matatu (3) mara ya mwisho kuzifuma nyavu za wapinzani ni mechi na Ruvu Shooting, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 
Mshambuliaji Laudit Mavugo pamoja na kupoteza ubora wake wa kuzifumania nyavu msimu huu, lakini ana mchango juu ya mafanikio ya Simba kwani amechungulia lango la wapinzani wao mara nne (4) na mechi yake ya mwisho kufunga ni dhidi ya Lipuli ya Iringa na kuisaidia timu yake kupata sare ya bao 1-1.
Beki Erasto Nyoni asiye na sekta maalumu ndani ya kikosi hicho, amefunga mabao matatu (3) na ndiye ameingia kwenye rekodi ya kuwanyima raha Yanga kwa msimu huu kwa kufunga bao la ushindi katika mechi yao na Wanajangwani.
Mghana Nicholas Gyan alikuwa kama mshambuliaji lakini kocha wa Simba sasa anamtumia kama beki amefanikiwa kufunga mabao mawili (2).
Mshambuliaji Juma Luizio, Mwinyi Kazimoto na Saidi Ndemla kila mmoja amefanikiwa kufunga bao mmoja hadi sasa.
Credit: Mwanaspoti