Rekodi mabao Ligi Kuu yamuweka mtegoni Lechantre


Dar es Salaam. Mabadiliko ya mbinu za uchezaji na ufundi yaliyofanywa na kocha Mfaransa Pierre Lechantre wa Simba katika siku za hivi karibuni, yameifanya timu hiyo kupunguza kasi ya kufunga mabao kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Tangu timu hiyo ilipotoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya Stand United, safu yake ya ushambuliaji imeonekana kupungua nguvu kwa kufunga idadi ndogo ya mabao kulinganisha na miezi ya mwanzoni mwaka huu.
Katika mechi tano Simba ilizocheza kwenye Ligi Kuu tangu ilipokutana na Stand United, imefunga mabao tisa ambayo ni wastani wa bao 1.8 kwa kila mechi, wakati katika mechi tisa ilizocheza kabla ya hapo iliweka wavuni 29 ambayo ni wastani wa mabao 2.9 kwa kila mchezo.
Mabadiliko yanayoonekana kuchangia kupunguza idadi ya mabao Simba yametokana na kutokuwa na kiungo mshambuliaji asilia (namba nane).
Lechantre amekuja na mfumo mpya kwa kumpanga kiraka anayecheza nafasi za ulinzi, Shomari Kapombe kucheza kwenye eneo hilo.
Mbinu hiyo imeboresha Simba kuwa imara katika kuibana timu pinzani isitengeneze nafasi za mabao, lakini imepunguza ubunifu wa kutengeneza nafasi nzuri za mabao kama ilivyokuwa zamani kabla ya ujio wa Mfaransa huyo.
Lengo la kumpanga Kapombe nafasi ya kiungo mshambuliaji katika mfumo 3-5-2 ni kuipa uimara kwenye safu ya kiungo upande wa kuzuia.
Kitendo cha kuwaweka benchi wachezaji wa kiungo asilia Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto au Mzamiru Yassin kumechangia kupunguza idadi ya mabao.
Simba inaonekana kutegemea zaidi mabao yanayotokana na mipira iliyokufa au jitihada binafsi za washambuliaji mapacha John Bocco na Emmanuel Okwi.
Nyota hao wakati mwingine wanalazimika kutumia nguvu kusaka mipira nje ya eneo la hatari la timu pinzani kutokana na kutopewa huduma sahihi kutokea kwenye safu ya kiungo.
Ni kama Mfaransa huyo amefanya mageuzi ya moja kwa moja ya mbinu zilizokuwa zikitumiwa na msaidizi wake Masoud Djuma ambaye kwa muda mfupi alioongoza, timu hiyo ilikuwa tishio kwa kutengeneza idadi kubwa ya nafasi za mabao na kufunga.
Katika mechi tatu Djuma alizoongoza Simba dhidi ya Ndanda FC, Singida United na Kagera Sugar, ilifunga mabao manane ambayo ni wastani wa mabao 2.7 na katika mechi 11 ambazo Lechantre alikuwa kwenye benchi, Simba imefunga mabao 26 ambayo ni wastani wa mabao 2.5 kwa kila mechi.
Hata hivyo, sehemu kubwa ya mabao 26 iliyofunga chini ya Lechantre, yalifugwa katika mechi ambazo timu hiyo ilimpanga kiungo asilia wa ushambuliaji tofauti na sasa.
Lechantre aliwahi kutetea uamuzi wa kumpanga Kapombe akidai ana uwezo mkubwa katika kushambulia na kujilinda timu inapopoteza mpira.
“Kocha ni mgeni amekuja katika kipindi Simba inahitaji ubingwa wa Ligi Kuu, pengine presha ya kupata matokeo ndiyo inamfanya aone bora kujaza idadi kubwa ya wachezaji wa nafasi za ulinzi,”alisema kocha msaidizi wa Taifa Stars, Hemed Morocco.
Chanzo: Mwanaspoti
MaoniMaoni Yako