Rekodi 2017/18 Yanga inatisha


KIPIGO cha juzi cha bao 1-0 kutoka kwa Mwadui FC, kimeifanya Yanga kucheza michezo tisa bila ya ushindi tangu kuondoka kwa kocha wake mkuu, Mzambia George Lwandamina na hivyo msimu huu wa 2017/18 kuonekana kuwa mbaya zaidi ukilinganisha na misimu minne iliyopita.
Kwa takriban misimu minne iliyopita, Yanga imekuwa ikishika nafasi ya kwanza ama ya pili, na haijawahi kupoteza mfululizo kwa idadi kubwa kama msimu huu. 
Pia imeambulia vipigo vitano, vikiwamo vitatu mfululizo kwenye michezo yake ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga ambayo msimu huu imeambulia patupu, imefungwa michezo mitano na kutoka sare mechi nne  kuanzia Aprili 7, mwaka huu.
Ushindi wake wa mwisho ilikuwa kwenye mchezo wake wa Kombe la Shirikisho kuwania kutinga hatua ya makundi dhidi ya Welayta Dicha ya Ethiopia.
Baadaye ilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Simba, pia ikaangukia kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Tanzania Prisons, ikafungwa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar na kipigo cha juzi cha bao 1-0 kutoka kwa Mwadui FC.
Kocha wa timu hiyo kwa sasa, Shadrack Nsajigwa, aliiambia Nipashe kuwa, amekuwa akikiandaa kikosi chake kwa ajili ya ushindi, lakini wamekuwa wakipata matokeo tofauti.
"Matokeo yanaumiza, lakini ndio mpira, tumekuwa tukijipanga kwa ajili ya ushindi ingawa mwisho wa siku tunapoteza mchezo," alisema Nsajigwa.
Alisema matokeo hayo mbali na kuwaumiza mashabiki wao, lakini pia yanawaumiza wao kama makocha hata wachezaji wake.
"Hakuna anayependa au kuyafurahia matokeo haya, yanaumiza, lakini hii ni changamoto na tunatakiwa kufanyia kazi mapungufu yetu," aliongezea kusema.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kuendelea kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa nyuma ya mabingwa Simba na Azam FC wanaoshika nafasi ya pili. 
Credit: IPP Media
MaoniMaoni Yako