Pluijm aahidi kuwaachia Singida United taji kama Yanga
Kocha Hans Pluijm amewahakikishia mashabiki na uongozi wa klabu hiyo kuwa amejipanga kutwaa Kombe la Shirikisho katika mechi itakayowakutanisha na Mtibwa Sugar wikiendi hii.


Pluijm aliyejiunga na kikosi cha Singida United mapema mara baada ya timu hiyo kupanda daraja daraja msimu uliopita wa 2016/17, alitokea katika klabu ya Yanga na amesema kuwa hana mashaka na kutwaa ubingwa wa FA kwani si mara yake ya kwanza.


“Ubingwa wa Kombe la Shirikisho tayari ni kama tunalo kwani si mara yangu ya kwanza kikosi ninachokifundisha kutwaa ubingwa ikiwemo kama ilivyokuwa kwa Yanga. Hivyo na wapenzi wa Singida United wajiandae kupokea kombe.”


Kocha Pluijm amesema hayo baada ya kumalizika kwa mazoezi ya kikosi chake katika Uwanja wa Field force ulioko kwa Mrombo nje kidogo ya Jiji la Arusha iliyowajumuisha wachezaji 16.


Amesema kuwa ari na moyo walionayo wachezaji wake katika mazoezi anaamini ubingwa tiyari ni wao huku akifurahishwa zaidi ya hali ya hewa ya ubaridi ulioko jijini hapa.


“Kwa mazingira ya Arusha na uwanja wa Sheik Amri Abeid tunakocheza ni dhahiri ni mazingira rafiki kwa soka kwa timu yoyote duniani si Tanzania tu hivyo na mimi nimefurahia hali hii na kikosi changu nao wameanza kuzoea kama ilivyokuwa lengo letu kuwatanguliza mapema.”
MaoniMaoni Yako