Okwi awomba radhi Simba kukosa penalti


KUFUATIA kukosa penalti kwenye mchezo wa juzi dhidi ya Kagera Sugar, mshambuliaji wa Simba na kinara wa mabao kwenye Ligi Kuu, Emmanuel Okwi, amewaomba radhi mashabiki wa timu hiyo kwa kukosa tuta hilo ambalo lingewaepusha na kipigo.

Simba juzi ilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu uliohudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli.
Kipigo hicho kinakuwa cha kwanza kwa Simba tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu inayoelekea ukingoni, wakati huu ikiwa imeshuka dimbani mara 29.
Akizungumza na Nipashe, Okwi alisema anajisikia vibaya kuona amekosa penalti muhimu ambayo ingeendeleza rekodi yao ya kucheza msimu huu bila kufungwa.
Alisema kwa niaba ya wachezaji wenzake, anaomba radhi kwa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kwa kuwa lengo lao lilikuwa kumaliza msimu bila kupoteza mchezo wowote mara baada ya kutwaa ubingwa.
Simba ilitangaza ubingwa ikiwa na michezo mitatu mkononi na hiyo ilitokana na Yanga ambao walikuwa wapinzani wao wakubwa kupoteza mchezo dhidi ya Tanzania Prisons kwa mabao 2-0.
"Tumeumia kama wachezaji, haikuwa lengo letu na hasa mimi kitendo cha kukosa penalti ambayo ingebadilisha matokeo, tutajitahidi kuhakikisha mchezo ujao ambao utakuwa wa mwisho tunamaliza vizuri," alisema Okwi.
Simba sasa itasafiri mpaka mjini Songea kucheza na Majimaji kwenye mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu mwishoni mwa wiki.
Credit: IPP Media
MaoniMaoni Yako