Okwi akubali ya Magufuli Simba


  • ***Atoa mbinu za mafanikio Afrika, mbeleko aachiwa Mo...
HUKU akiwa na machungu ya kukosa penalti katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar, mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, amesema anaungana na Rais Dk. John Magufuli, kuwa muda umefika kwa timu yake kujipanga kuutwaa ubingwa wa Afrika.
Rais Magufuli aliitaka Simba ijipange kutwaa ubingwa wa Afrika na kuweka wazi kuwa kwa kiwango alichokishuhudia dhidi ya Kagera Sugar katika Uwanja wa Taifa, Simba haiwezi kufika mbali katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, ndio mabingwa wapya wa Bara wakiwa wamebakiza mchezo mmoja wa funga dimba ambao utachezwa ugenini dhidi ya Majimaji ya Songea.
Akizungumza na Nipashe jana, Okwi, alisema kushinda taji la ubingwa wa Afrika ndio lengo lake kwa msimu ujao na anaamini Simba inaweza kuutwaa endapo itakubali kuwekeza kama klabu nyingine za bara hili zilivyowekeza.
Okwi alisema katika soka hakuna kinachoshindikana na kikubwa ni kukubali kwamba mafanikio yanatokana na uwekezaji wa hali ya juu.
"Namshukuru Mungu tumetimiza lengo la kutwaa ubingwa wa Tanzania, haikuwa kazi rahisi, ushirikiano wetu ndio umetufikisha hapa,  kwa sasa lengo langu ni kuona ninalibeba taji la Afrika," alisema mshambuliaji huyo raia wa Uganda.
Alisema anajua kuna changamoto mbalimbali katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini umakini na kujituma kwa wachezaji ndiyo siri pekee itakayowapa mafanikio.
Okwi pia ameshabeba taji la Kombe la Chalenji (Afrika Mashariki na Kati) mara kadhaa akiwa na timu yake ya Taifa ya Uganda (Cranes) na sasa anataka kuweka historia hiyo ambayo washambuliaji wawili wa Tanzania, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu waliiweka wakiwa na TP Mazembe ya Kongo.
Mganda huyo ameisaidia Simba kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara ambalo walilikosa kwa misimu minne mfululizo kwa kufunga mabao 20 huku nahodha wa Wekundu wa Msimbazi, John Bocco, akifuatia katika orodha ya wafungaji kwa kupachika mabao 14.
Okwi alishindwa kuisawazishia timu yake bao baada ya kukosa penalti katika mechi waliyofungwa bao 1-0 na Kagera Sugar na kuwa mechi ya kwanza kupoteza msimu huu mbele ya Rais Magufuli ambaye alikwenda kwa ajili ya kuwakabidhi kombe la ligi Jumamosi iliyopita.
Hata hivyo, Simba inaweza kufanya vizuri kama ambavyo Magufuli anatamani siku moja kupokea ubingwa wa Afrika kutoka kwa timu za Tanzania, endapo mchakato mzima wa klabu hiyo kuendeshwa kibiashara zaidi (mfumo wa hisa), utakamilika mapema baada ya juzi wanachama wa Simba kuridhia mabadiliko ya katiba.
Kukamilika kwa mchakato huo, kutamfanya  mfanyabiashara Mohamed 'Mo' Dewji kumiliki hisa asilimia 49 huku 51 zikibaki kwa wanachama.
Tayari Mo alishaahidi kujenga hosteli za kisasa, kusajili wachezaji wa kiwango cha juu pamoja na kuwa na kocha bora huku akihakikisha timu hiyo inakuwa na uwanja wake wa kisasa.
Credit: IPP Media
MaoniMaoni Yako