Wednesday, May 2, 2018

Nsajigwa: Sababu kipigo Yanga hii

Tags

YANGA juzi ilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa mahasimu wao Simba na kuwafanya mabingwa hao watetezi kuwa nyuma kwa pointi 14 wakati huu Ligi Kuu Bara ikielekea ukingoni.
Kocha msaidizi wa Yanga ambaye alibeba majukumu ya Kocha Mkuu, George Lwandamina aliyetimka klabuni hapo, amesema kipigo walichokipata juzi kimetokana na makosa yaliyokuwa yakifanywa na wachezaji wake hasa eneo la kiungo.
"Tulifanya makosa mengi, Simba walitumia mapungufu yetu kupata lile bao, hatukuwa vizuri kwenye eneo la kiungo, lakini pia safu ya ulinzi hatukuwa imara kwenye mipira ya krosi," alisema Nsajigwa.
Aidha, alisema mabadiliko aliyoyafanya ya kumtoa Papy Tshishimbi na Ibrahim Ajibu ambayo yalilalamikiwa na mashabiki wengi, yalikuwa ya kiufundi zaidi.
"Tshishimbi hakuwa kwenye ubora wake na hata Ajibu, tulifanya mabadiliko ya kuwatoa na kuwaingiza Mahadhi (Juma) na Buswita (Pius) ili kuongeza nguvu ya ushambuliaji," alisema Nsajigwa.
Alisema kwa kusaidiana na kocha mpya wa timu hiyo ambaye juzi hakuwa kwenye benchi kutokana na kutokamilika kwa vibali vya kufanyia kazi, Mkongoman Mwinyi Zahera, watafanyia kazi haraka mapungufu waliyoyaona.
"Tuna michezo ya Kombe la Shirikisho Afrika, tutahakikisha tunafanyia kazi kile tulichokiona ili kujiandaa vyema na mechi hizo na michezo mingine iliyobakia ya Ligi Kuu," alisema Nsajigwa.
Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa kama ilivyo kwa watani zao Simba,  itacheza mchezo wake wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger ya Algeria mwishoni mwa wiki hii.
Pia ina michezo mingine dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda na Gor Mahia ya Kenya ambazo wapo nazo kundi moja la michuano hiyo.
Chanzo: IPP Media