Ni Shangwe Kubwa Mtwara, Ndanda Yajinusuru Kushuka Daraja Ligi Kuu


Kikosi cha Ndanda kimeibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mwadui FC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara leo.

Mabao hayo yote yametiwa kimiani kipindi cha kwanza na Jacob Massawe mnamo dakika ya 3, Mrisho Ngassa kwenye dakika ya 5 na John Tiber katika dakika ya 40.

Matokeo ya mchezo huo yanaiweka Ndanda katika mazingira ya kusalia kwenye Ligi Kuu Bara kwa kufikisha pointi 26 na kupanda nafasi moja kutoka ya 15 mpaka ya 13.

Vita kubwa sasa imebaki kati ya Njombe Mji na Majimaji FC ambazo zina mazingira mabaya zaidi ya kuendelea kusalia kwenye ligi.

Ndanda imefikisha alama 26 ikiwa imesaliwa na mchezo mmoja ambao inahitaji kushinda ili kuweka asilimia 100 za kusalia kwenye ligi msimu ujao.
CREDIT: Saleh Jembe
MaoniMaoni Yako