Mtanzania aahidi medali Mbio za Dunia


Dar es Salaam. Mwanariadha, Francis Damas amesema ana matumaini ya kutwaa medali ya dhahabu kwenye mbio za dunia za vijana zilizopangwa kufanyika nchini Finland.
Damas atachuana Juni 16 katika mbio zitakazofanyika Jamhuri ya Czech kusaka viwango vya kushiriki mashindano ya dunia yaliyopangwa kuanza Julai 10 hadi 15.
Mwanariadha huyo ambaye ni mshindi wa medali ya shaba katika michezo ya Madola mwaka jana nchini Bahamas, anatarajiwa kuondoka nchini Juni 10 kwenda Czech.
“Niko vizuri naendelea na mazoezi ambayo nafanya kutwa mara mbili kwenye kambi yangu iliyopo Mbulu, naenda Czech kwa kazi moja ya kuleta medali,” alisema Damas.
Mwanariadha huyo anatarajiwa kuchuana katika mbio za mita 3000 na 5000 kwenye mashindano hayo na akifanya vyema ataiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya dunia ya vijana.
“Nafanya mazoezi kila siku nakimbia uwanjani kusaka spidi na barabarani kujenga pumzi kila siku mara mbili,” alisema Damas.
Kocha wa mwanariadha huyo, Meta Petro alisema maandalizi ya Damas yako katika hatua nzuri na ana matumaini ya kufanya vyema katika mashindano hayo.
MaoniMaoni Yako