Mrundi Simba afichua siri Yanga


YANGA juzi Alhamisi ilipoteza rasmi ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kutuma kikosi dhaifu jijini Mbeya kuvaana na Prisons na kulala mabao 2-0, lakini kumbe nyuma ya mpango huo Kocha Msaidizi wa Simba, Masudi Djuma anahusika mwanzo mwisho.
Ni hivi. Kocha huyo raia wa Burundi amefichua, Yanga haikupeleka kikosi dhaifu Mbeya kwa bahati mbaya ila ni wazo alilowapa kupitia kwa Kocha Msaidizi wao, Shadrack Nsajigwa kuwa awape nafasi wachezaji wasiocheza ili wale mastaa wa kikosi cha kwanza wapate muda wa kujiandaa vyema kwa mechi za kimataifa za CAF.
Akizungumza na Mwanaspoti, Djuma alisema alitoa ushauri kwa Nsajigwa siku walipoifunga timu hiyo bao 1-0 Uwanja wa Taifa.
“Niwe muwazi, ushauri wangu nilioutoa kwa kocha msaidizi wa Yanga ndio ambao nimeona ukifanyiwa kazi na benchi la ufundi la timu hiyo, kwani tulipowafunga bao 1-0 pale Taifa baada ya mechi nilizungumza na Nsajigwa nikamwambia kwa sasa waelekeze nguvu kwenye Kombe la Shirikisho Afrika kwani katika ligi hawana chao,” alisema.
Djuma anayemsaidia Mfaransa Pierre Lechantre alisema tofauti na wadau wanavyoiponda Yanga kwa ilichofanya Mbeya, walikuwa sahihi kwani wanapaswa kuelekeza nguvu katika mechi yao ya CAF dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda.
“Nawashangaa wanaiponda Yanga kutumia wachezaji wasio na nafasi kikosi cha kwanza wako sahihi, ndivyo walipaswa kufanya kwani wanatakiwa kukusanya nguvu zaidi ya kushinda kwenye mechi za kundi lao la Shirikisho Afrika,” alisema Djuma.
Kichapo ilichopewa Yanga kiliirahisisha kazi Simba ya kubeba taji la Ligi Kuu baada ya misimu mitano kwani pointi 65 ilizonazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote sasa.
Source: Mwanaspoti
MaoniMaoni Yako