Mo Salah atua Hispania, ampotezea RamosLondon, England. Wakati Mohamed Salah, amewasili nchini Hispania kwa matibabu, mshambuliaji huyo ‘amemsamehe’ nahodha wa Real Madrid Sergio Ramos.


Licha ya kuumizwa vibaya na kutishia ushiriki wake wa fainali za Kombe la Dunia, Salah hakumnyooshea kidole beki huyo.


Salah aliumia bega baada ya kuchezewa faulo na Ramos katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambao Real Madrid ilishinda mabao 3-1 dhidi ya Liverpool.


Mtaalamu wa viungo wa Liverpool, Ruben Pons, alisema mchezaji huyo hakumlaumu Ramos kwa tukio hilo lililotokea mjini Kiev, Ukraine.


Pons alisema licha ya maelfu ya mashabiki wa soka kumtolea maneno makali Ramos kwenye mitandao, lakini Salah hakutoa kauli yoyote dhidi ya beki huyo wa kati.


“Salah hakuniaeleza jambo lolote kuhusu Sergio Ramos, sidhani kama ana hasira naye. Ilikuwa ni sehemu ya ajali,”alisema Pons.


Alisema muda mfupi baada ya kuumia, alimuahidi jopo la madaktari wa klabu hiyo watapambana kuhakikisha anapona haraka kuwania fainali za Kombe la Dunia.


Pons alisisitiza timu ya madaktari Liveropool itafanya kazi kwa kiwango bora na matumaini yao ni kumuona mchezaji huyo wa kimataifa wa Misri anarejea uwanjani haraka.


Hata hivyo, Pons alisema Salah anaweza kuwa nje ya uwanja wiki tatu hadi nne, lakini watapambana kupunguza idadi ya siku ili kuwahi fainali hizo nchini Russia.


Awali, Salah aligoma kuzungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili Hispana kwa matibabu.


Salah alikuwa kimya licha ya kuulizwa maswali na waandishi wa habari waliokwenda uwanja wa ndege.


Misri inatarajiwa kufungua pazia la mashindano hayo kwa kupepetana na Uruguay Juni 15 kabla ya kuzivaa Saudi Arabia na Russia.
MaoniMaoni Yako