Mo Ibrahim akana kuteta na Yanga

KIUNGO mshambuliaji wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, Mohamed Ibrahim "Mo Ibrahim" amekanusha kufanya mazungumzo ya kujiunga na Yanga kwa ajili ya msimu ujao kama ambavyo inaelezwa katika vyombo mbalimbali vya habari.

Mo Ibrahim ambaye ana mkataba na Simba unaomalizika mwakani, amekiri kufuatwa na viongozi wa timu mbalimbali, lakini bado hajafikia uamuzi wa kuondoka katika kikosi cha mabingwa hao wapya.
Kiungo huyo alisema anaamini akiwa na Simba atatimiza ndoto zake ambazo bado hazijatimia mpaka sasa baada ya kutua klabuni hapo akitokea Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
"Kuna andiko linasambaa 'facebook' kuwa ninampango wa kuondoka, ile sio akaunti yangu, siitambui, kiukweli bado ninaipa Simba nafasi ya kwanza na endapo kama wao hawatanihitaji ndio nitaangalia klabu nyingine," alisema kiungo huyo.
Naye Meneja wa kiungo huyo, Jamal Kisongo, amesema Mo bado ni mchezaji halali wa Simba na kama kuna mtu ambaye anafanya mazungumzo naye atakuwa anakosea.
Alisema ni vyema klabu zikaheshimu utaratibu katika mchakato wa usajili na hii itawasaidia kuwapunguzia adhabu wachezaji na kuzipa wakati mgumu timu zitakapowakosa wachezaji waliowasajili kimakosa.
Hata hivyo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), halijafungua rasmi dirisha la usajili, lakini klabu zimeshaanza kusaka nyota wapya ili kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano mingine mbalimbali.
Ligi Kuu Bara msimu ujao itashirikisha klabu 20 kutoka mikoa mbalimbali, 14 zilizobaki na sita mpya ambazo zimepanda daraja.
Credit: IPP Media
MaoniMaoni Yako