Mgahawa Kenya watoza dola 10,000 kutazama harusi ya Prince Harry na Meghan Markle.

Mgahawa mmoja jijini Nairobi imezua mjadala mtandaoni Kenya baada ya kutangaza hafla ya kufuatilia harusi ya mwanamfalme wa Uingereza Harry na Bi Meghan Markle ambapo wanaotaka kushiriki watalipa Sh1 milioni (dola 10,000 za Marekani).
Mgahawa huo wa Windsor Golf Hotel and Country Club umeandaa hafla hiyo kwa ushirikiano na runinga ya kibinafsi ya KTN na kampuni inayangazia masuala ya sherehe za harusi ya Samantha's Bridal.
Watakaohudhuria sherehe hiyo wanatakiwa kuvalia mavazi ya harusi. Chakula kitapikwa kwa mtindo wa Kiingereza.
Sherehe hiyo itafanyika saa tano unusu asubuhi hadi saa kumi na moja jioni ambapo watakaohudhuria watatumbuizwa na kufahamishwa kuhusu yatakayokuwa yakiendelea katika harusi hiyo.
Tangazo la hafla hiyo limedokeza kwamba wachumba watasafirishwa kwa helikopta hadi Mlima Kenya ambapo wataweza kujionea jua likichomoza kileleni na kula kiamsha kinywa.
Tangazo hilo hata hivyo halijaeleza iwapo ni wote watakaohudhuria watakaonufaika na huduma hiyo.
Gazeti la Nation limewanukuu waandalizi wakisema kwamba wanalenga kuwapata wachumba 20 hivi, na kwamba hawataki watu wengi.
Gazeti hilo linasema kufikia Jumamosi waandalizi walisema kulikuwepo na nafasi zilizokuwa wazi.
Baadhi ya Wakenya mtandaoni wamekuwa wakishangaa ni vipi mtu anaweza kutumia dola 10,000 milioni 'kutazama sherehe kupitia runinga' ilhali pesa hizo zinatosha kugharimia safari ya kwenda hadi Kasri la Windsor na kushuhudia harusi hiyo moja kwa moja.
Nauli ya ndege kutoka Uwanja wa Jomo Kenyatta Nairobi kwenda uwanja wa Heathrow Ijumaa, viti vya kawaida gharama yake ni kati ya dola 527-610 kwa mtu mmoja, na kurudi 20 Mei kati ya dola 640-699 kwa mujibu wa makadirio ya nauli ya shirika la ndege la Kenya, Kenya Airways.
Teksi kutoka Heathrow kwenda Windsor ni kati ya $40-68.
Malazi (Chumba cha wageni wawili, usiku mmoja pamoja na chakula) ni kati ya £140-695.
Hata hivyo, kwa sasa hoteli nyingi za karibu na hapo zimejaa wageni.
Familia ya Kifalme imeruhusu wageni 1,200 hivi pekee kuhudhuria sherehe hiyo, maana kwamba ingawa watakaofika eneo hilo huenda wakawa wengi, ni wachache sana watakaohudhuria sherehe hiyo na kuwaona bi harusi na bwana harusi kwa macho yao.
Baadhi wanaamini gharama hiyo ni ya juu mno.
Miaka ya karibuni, imekuwa kawaida kwa hoteli na kampuni mbalimbali kuandaa sherehe na huduma za kifahari wakiwalenga wapenzi na wachumba.
Mapema mwaka huu, mgahawa wa Villa Rosa Kempinski, Nairobi uliandaa huduma ya Sh5.4 milioni kwa wapenzi ambao wangekaa chumbani kwa siku tatu Siku ya Waendanao.

MaoniMaoni Yako