Wednesday, May 2, 2018

Mbao yapambana kubaki Ligi Kuu kuzisulubu Simba, Yanga

Tags

kikosi cha Mbao fc
MWANZA. PAMOJA na kupata matokeo yasiyoridhisha Mbao FC kwenye mechi zake za Ligi Kuu, Kocha wa timu hiyo, Novatus Fulgence amesisitiza kuwa kamwe hawatashuka daraja.
Kocha Fulgence amekiongoza kikosi hicho katika mechi mbili na kuambulia pointi moja waliyoipata dhidi ya Majimaji kabla ya kuchezea kichapo cha bao 1-0 mapema wiki hii kutoka kwa Mwadui.
Mbao FC imeibuka kuwa miongoni mwa timu tishio hasa ilipokutana na Simba au Yanga katika moja ya mechi zake za Ligi Kuu.
Hadi sasa timu hiyo yenye maskani yake Ilemela jijini hapa imekusanya pointi 24 na kukaa nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu baada ya kucheza mechi 26.
Fulgence alisema kuwa licha ya kutopata matokeo mazuri kwenye mechi mbili alizosimamia, timu haitashuka daraja kwani makosa aliyobaini atayafanyia kazi.
Alisema kuwa kikubwa ni kuwaandaa vyema vijana kisaikolojia na kiushindani ili kuhakikisha mechi zilizobaki wanapambana kufa na kupona kusaka ushindi.
“Wadau na wapenzi wa timu watulie, Mbao haishuki Daraja,makosa tuliyoyafanya katika mechi zilizopita tutayafanyia kazi ili michezo ijayo tuweze kushinda”alisema Fulgence.
Kocha huyo wa zamani wa Taifa Stars,alisema kuwa kwa sasa Ligi ni kama ndio imeanza,hivyo kila mchezo ni fainali kwao na hawatakubali kupoteza chochote.
“Ligi ni kama imeanza upya kwetu,hizi mechi nne tutapambana kuhakikisha hatupotezi hata mmoja,vijana  wana uwezo,kikubwa ni kufuata maelekezo na kutuliza presha,”alisema Kocha huyo.
Chanzo: IPP Media