Mbao FC wapigwa butwaa zali la kubaki Ligi KuuMwanza.Baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Bara, benchi la ufundi la Mbao FC limesema kuwa haikuwa kazi rahisi kukwepa rungu la kushuka daraja licha ya kujinusuru dakika za mwisho.


Mbao ilinusurika kushuka daraja baada ya kukusanya pointi 31 na kukaa nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi hiyo iliyomalizika juzi Jumatatu,ambapo Njombe Mji na Majimaji ndizo zilishuka daraja.


Meneja wa Klabu hiyo, Faraji Muya alisema kuwa kubaki kwao Ligi Kuu msimu ujao,haikuwa kazi rahisi kutokana na ushindani uliokuwapo kwa timu shiriki.


Alisema kuwa licha ya kujinusuru dakika za mwisho,lakini wanashukuru kufikia malengo yao ya kutoshuka na kwamba kwa sasa wanaenda kujipanga kuhakikisha msimu ujao wanafanya vizuri.


“Ligi ilikuwa ngumu kwa timu zote kuonyesha ushindani,lakini kikubwa tunashukuru kuweza kukwepa kushuka daraja licha ya kujinusuru dakika za mwisho”alisema Muya.


Meneja huyo aliongeza kuwa mapungufu yaliyojitokeza watakaa na kutathimini kujua wapi waanzie ili ligi ikianza wawe fiti na yasijirudie ya kusaka ushindi wa kujinusuru kushuka daraja mechi za mwisho.


“Tunaenda kujipanga upya na kufanya tathmini kuangalia wapi tumeshindwa ili msimu ujao tuweze kufanya vizuri na isijirudie ya kusubiri matokeo ya dakika za mwisho,” alisema Meneja huyo.
MaoniMaoni Yako