Maxime: Tumekuja 'kuitibulia' Simba SC

KIKOSI cha Kagera Sugar kilitarajiwa kuwasili Dar es Salaam jana usiku huku Kocha wake Mkuu, Mecky Maxime, akisema kuwa amekuja jijini kwa kazi moja ya "kuvuruga na kutibua" sherehe za ubingwa kwa kuvunja rekodi ya kutofungwa wanayoishikilia.


Kagera Sugar ambayo haikuanza vyema msimu huu, sasa ina pointi 31 na iko katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na mechi mbili mkononi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Maxime, alisema kuwa wachezaji wake watawakabili mabingwa hao wapya, Simba bila hofu yoyote ya baada ya kuondoka kwenye janga la kushuka daraja.
Maxime alisema sasa wanajiandaa kuonyesha soka la "shule" na anaamini kama washambuliaji wake watakuwa watulivu, wana uwezo wa kuifunga Simba ambayo haijafungwa mechi hata moja msimu huu.
"Maneno yamekuwa mengi, sisi ndio Kagera Sugar na wanatujua, tumekuja kuwavuruga, tunachojitaji ni kutumia vyema nafasi za kufunga, kwa mfano mechi ya Mbeya City, tulitengeneza nafasi 10, ila bahati mbaya hatukushinda," alisema kocha huyo.
Baada ya kuivaa Simba Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, siku ambayo mabingwa hao watakabidhiwa kombe lao, Kagera Sugar itasafiri kuelekea Iringa kuwafuata wenyeji Lipuli FC kwa ajili ya mechi ya kufunga pazia la ligi itakayofanyika Mei 28, mwaka huu.
Credit: IPP Media
MaoniMaoni Yako