Maxime: Sitausahau msimuu huu

WAKATI pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara likiwa linaelekea ukingoni, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amesema kamwe hatausahau msimu huu wa 2017/18 katika maisha yake.

Kagera Sugar ambayo imebakiza mechi moja dhidi ya Lipuli, ilikuwa katika timu zilizoko kwenye janga la kushuka daraja, ikiwa imevuna pointi 13 katika mzunguko wa kwanza na pointi 23 kwenye mzunguko wa lala salama.
Akizungumza na gazeti hili jana, Maxime, alisema msimu huu ulikuwa na ushindani na changamoto zaidi kuliko misimu iliyopita ambayo kupata pointi uwanjani ilikuwa kazi rahisi.
Maxime alisema kwa upande wa kikosi chake, wachezaji walikuwa wakipambana, lakini hawakuwa na bahati ya kushinda na hivyo mechi nyingi kuambulia sare au kufungwa.
"Sitausahau msimu huu, ulikuwa mgumu, wachezaji walipambana na kucheza vizuri, lakini mwisho wa mechi hatukupata pointi, hali ilikuwa mbaya zaidi katika mzunguko wa kwanza, tulimaliza tukiwa na pointi 13 tu," alisema Maxime.
Aliongeza kuwa kwa upande wa mbio za ubingwa, Simba ilionekana iko vizuri mapema huku baadhi ya timu zikiwa zimekata "pumzi" na kuipa nafasi ya kuendelea kujiimarisha kwenye mbio hizo na hatimaye kufanikiwa kubeba taji. 
Credit: IPP Media
MaoniMaoni Yako