Matatizo haya yakitatuliwa, Yanga mbona itapeta

MWENENDO wa Yanga hauridhishi kwa sasa. Mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara wamecheza michezo minne mfululizo sasa bila kupata ushindi, ikiwa ni rekodi mbovu zaidi kwao tangu kuanza kwa msimu huu.
Yanga ilipoteza mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika ugenini kwa Welaytta Dicha, kabla ya kutoka sare na Singida United na Mbeya City na kisha kupoteza bao 1-0 kwa Yanga.
Mwenendo wa timu hiyo kwa sasa umezua hofu juu ya uwezekano wa timu hiyo kufanya vizuri kwenye mechi za hatua ya makundi za kombe la Shirikisho, ambapo inaanzia ugenini dhidi ya USM Algers Jumapili ya wiki hii.
Hakuna ubishi kwamba kwa sasa kuna matatizo ambayo yanaiandama timu hiyo ambayo kama yasipopatiwa ufumbuzi, huenda ikatia aibu kwenye mechi hizo za Afrika n ahata zile za Ligi Kuu zilizosalia.

Madeni ya mishahara
Asikudanganye mtu, hakuna mwanadamu ambaye atafanya kazi bila kulipwa. Hiyo ni tangu enzi na enzi. Wachezaji wa Yanga wamekuwa wakisotea mishahara yao kwa miezi kadhaa sasa jambo ambalo limeshusha morali yao.
Yanga ni timu kubwa. Ni mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu na pia timu yenye mashabiki wengi nchini. Wachezaji wa Yanga hawapaswi kukaa miezi miwili ama mitatu bila kulipwa. Inawapunguzia hali ya kujiamini.
Kwa sasa timu hiyo inapaswa kusaka fedha kwa udi na uvumba ili kupunguza madeni hayo ya mishahara, vinginevyo mambo yatazidi kwenda mrama.

Hamasa ya uongozi
Uongozi wa Yanga kwasasa ni kama vile haupo. Kazi zote ni kama vile ameachiwa Charles Mkwasa ambaye ni mwajiriwa tu wa timu hiyo. Msaada wa viongozi wa kuchaguliwa umekuwa mdogo sana klabuni hapo.
Viongozi wenyewe ndio hawa kina Salum Mkemi, timu yao ina matatizo lukuki, wao wanapiga tu kelele mtaani na vijembe huko Instagram. Viongozi wa timu kama Yanga wanapaswa kuwa watu wa mikakati. Watu wenye mipango.
Uongozi wa Yanga umepwaya kuanzia juu kwa Kaimu Mwenyekiti, Clement Sanga. Ukapwaya pia kwa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji. Uongozi huu usipobadilika, Yanga itapoteza tu muda.

Kitengo cha matibabu
Kitengo cha matibabu cha Yanga kimepwaya sana msimu huu. Wachezaji wengi wamekuwa wakiumia na kushindwa kurejea uwanjani kwa wakati. Mfano, Donald Ngoma na Amissi Tambwe wamekuwa majeraha wa muda mrefu wa timu hiyo, huku kitengo cha tiba cha timu hiyo kikitoa taarifa za uongo juu  yao kila siku.
Kitengo hicho kinahitaji maboresho vinginevyo timu hiyo itaendelea kupoteza wachezaji wazuri. Andrew Vincent ‘Dante’, Thaban Kamusoko, Beno Kalolanya ni miongoni mwa wachezaji ambao wamekuwa na majeraha mara kwa mara.

Usajili wa nguvu
Timu hiyo inahitaji kufanya maboresho makubwa ya timu hiyo, ikiziba maeneo yote yenye upungufu. Eneo la kwanza ni safu ya ushambuliaji ambayo imeachwa kama yatima kwa Obrey Chirwa ambaye ndiye amekuwa akiibeba timu hiyo msimu huu.
Ibrahim Ajibu amekuwa kwenye kiwango cha kawaida tofauti na matarajio ya mashabiki wa timu hiyo. Ngoma na Tambwe hawana tena uwezo wa kuibeba timu hiyo kutokana na majeruha ya mara kwa mara.
Timu hiyo inahitaji mawinga wawili wa maana ambao watakuwa na kiwango kinachokaribiana na aliyekuwa staa wao, Saimon Msuva kwani Geofrey Mwashiuya na Juma Mahadhi wameshindwa kabisa kazi hiyo.
Pia anahitajika kiungo mbadala wa Thaban Kamusoko ambaye naye majeraha yamemfanya awe mchezaji wa kawaida msimu huu. Maeneo hayo ni muhimu sana, vinginevyo Yanga itaendelea kupoteza muda.
Chanzo: Mwananchi
MaoniMaoni Yako