Mastaa Simba wawaalika Yanga siku ya kukabiziwa kombe


Baada ya Simba kuwa mabingwa wa ligi kuu,  basi bwana wachezaji wao wanatamba  kupita kiasi na sasa wamewakaribisha Watani wao wa jadi Yanga wafike kwa wingi siku watakayo kabidhiwa Kombe lao.
Kiungo wa timu hiyo, Mzamiru Yassin amesema, wao wameshamaliza kazi na sasa wanawaachia Yanga na Azam FC wapambane na hali zao huko chini.
"Kazi iliyobaki kwetu ni kuweka historia tu ya kumaliza bila kufungwa na si kuumiza kichwa tena hayo ni ya  Yanga na Azam kumpata nani atakayemaliza kwenye nafasi ya pili,"anasema Mdhamiru ambaye alisajiliwa na Simba akitokea Mtibwa Sugar.
Jonas Mkude ni miongoni mwa wachezaji waliodumu kikosini hapo tangu Simba ilipoutema ubingwa mwaka 2012, amezungumzia mafanikio ya sasa ni faraja kwake.
"Nimeamini wanaosema kimya kingi kina kishindo. Kitendo cha Simba kutochukua ubingwa kwa muda mrefu ilikuwa changamoto kubwa lakini sasa ni furaha, tumewafunga Yanga, tumewapita kwa idadi ya mabao, pointi na sasa tunapambana tusipoteze mchezo hata mmoja," amesema na kuongeza.
"Unajua kila kitu kina wakati wake, Yanga walitamba na kujiona wao ndio wamiliki wa taji hilo lakini sasa imeisha ni wakati wetu na tunawakaribisha wajitokeze kwa wingi siku tutakayokabidhiwa Kombe."
Nahodha wa kikosi hicho, John Bocco aliyefunga mabao 14, amesema anajiona mwenye bahati kutua kwenye kikosi cha Simba sambamba na kunyakua taji la ubingwa.
"Ni faraja kwa mchezaji anapokaa kwenye timu na akaacha historia ya kukumbukwa, si kitu kidogo ambacho tumekifanya Simba
kwa msimu huu, si jambo dogo, kutua Simba na kufanikisha ubingwa,  kilichobakia ni mtazamo mpya wa kimataifa, imefika wakati wa timu zetu kufanya kitu cha tofauti," amesema Bocco.
Credit: Mwanaspoti
MaoniMaoni Yako