Maisha mapya Prof. Muhongo jimboni akipigania zahanati za wapiga kura

  •  Atinga kila kona kuhamasisha ‘hapa kazi’
  •   Mzimu mkuu ‘kujitolea kwa hali na mali’
  • Vita kuu ni vituo vya afya 20, zahanati 39
MWANZONI katika duru za siasa, huyu alikuwa maarufu sana katika nafasi ya Waziri wa Madini na Nishati, kwa awamu mbili zinazoambatana.
Wakati katika serikali ya Awamu ya Nne alikuwa mbunge wa kuteuliwa, safari hii Awamu ya Tano, amekuwa Mbunge wa Musoma Vijijini.

Huyu ni mwanajiolojia, Profesa Sospeter Muhongo, aliyetumikia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na nafasi nyingine nje ya nchi.
Mtikisiko wa kiutawala nchini katika sekta ya nishati na madini, ulimlazimisha kuliacha Baraza la Mawaziri.

Ukimya wake wa muda mrefu kiasi tangu hapo, una siri ya kuhamisha juhudi na stadi za utendaji wake unaojulikana kwa wengi, hivi sasa ukiwa jimboni akipambana.

Operesheni kuu aliyonayo sasa mkononi ni kuboresha afya za waliompigia kura, kupitia Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM), yenye wastani wa muongo mmoja.

MMAM inalenga kila kijiji kuwa na zahanati na kata kuwa na kituo cha afya, juu yake katika ngazi ya wilaya kunakuwapo hospitali na katika mkoa kuna hospitali ya rufani.
  
Kimsingi, Musoma Vijijini ni miongoni mwa majimbo 10 yaliyomo mkoani Mara, likiundwa na kata 21 zenye vijiji 68, baada ya kugawanywa mwaka 2015 na kupatikana jimbo lingine la Butiama.

Kwa maana hiyo, katika utekelezaji wa MMAM, jimboni Musoma Vijijini, kuna pengo la zahanati 31 ambayo ni sawa na asilimia 57.35 ya lengo la kila kijiji kuwa na zahanati moja. Hadi sasa kuna jumla ya zahanati 29 ambayo ni hitaji la asilimia 42.65 tu.

Pia, kwa vituo vya afya jimboni humo kimoja, wakati hitaji halisi ni katika kila kata, jumla yao ni 21. Hiyo inafanya jimbo la Musoma Vijijini limetimiza hitaji la asilimia 4.76 pekee ya hitaji lote.

Kwa mujibu wa mbunge Profesa Muhongo, harakati zinazoendelea sasa ni kukamilisha zahanati tisa, kati ya hitaji la zahanati 39.

Anasema, katika kujinusuru na uhaba mkubwa wa vituo vya afya, kipo kimoja kinachojengwa cha Nyambono, huku zahanati mbili zinakarabatiwa na kufanyiwa upanuzi zipandishwe adhi viwe vituo vya afya, akivitaja vya vijiji vya Mugango na Bukima.

Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 wakazi wa jimbo hilo walikuwa ni 216,409, wanaume wakiwa ni 106,163, na wanawake 110, 246, lakini kwa sasa ikadariwa kuwa idadi ya watu imeongezeka kufikia 227,230.
Ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Kurwaki, ukiendelea wiki hii.
Changamoto

Profesa Muhongo, anadokeza Musoma Vijijini ina jumla ya zahanati 29 (asilimia 42.65 ya mahitaji) zinazofanya kazi, huku nyingine zikiendelea kujengwa katika vijiji mbalimbali.

Pia, anasema wana kituo kimoja cha afya kilichopo kijiji cha Murangi, ambacho wakazi wa vijiji mbalimbali jimboni humo wamekuwa wakikitumia kupata huduma ya afya.

"Ukiangalia idadi ya vijiji na idadi ya zahanati na vituo vya afya, utagundua kwamba bado kuna uhitaji mkubwa wa kuwa na zahanati nyingi zaidi na vitu hivyo, ili kusogezea huduma za afya karibu na wananchi," anasema Profesa Muhongo. 
Anasema lengo lake kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vijijini, ni kwamba kila kijiji kinapaswa kuwa na zahanati kama inavyoelekeza MMAM.

Profesa Muhongo anazitaja zahanati ambazo ujenzi wake unaendelea, ni pamoja na: Kijiji cha Mkirira katika kata ya Nyegina; Kurwaki, kata ya Mugango; na zahanati Kijiji cha Butata, Kata ya Bukima; Chirorwe, Kata ya Suguti; Kigeraetuma, kata ya Nyakatende; na Mmahare, kata ya Etaro, huku zahanati ya kijiji cha Mwiringo, katika kata ya Busambara imeshaanza kufanya kazi.

"Mbali na ujenzi wa zahanati, kuna kituo kipya cha afya cha Nyambono, ambacho ujenzi wake ulianza Desemba mwaka jana, pia tunapanua zahanati za vijiji vya Mugango na Bukima kuwa vituo vya afya," anaeleza.

Mbunge huyo anasema vituo hivyo vitatu vikikamilika, jimbo lake litakuwa na vituo vinne vya afya na kwamba mkakati wake ni kutaka kila kata iwe na kitu cha afya, ili angalau kukidhi mahitaji ya huduma ya afya.

Profesa Muhongo anasema binafsi huwa anaumia anapoona kazi jimboni mwake wakitembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya kutoka sehemu nyingine, ndio maana ameamua kuhamasisha ujenzi wa zahanati na vituo vya afya.

"Kwa mfano, vijiji vitatu vinavyounda Kata ya Musanja havina zahanati. Watu wamekuwa wakitembea umbali wa kilometa zaidi ya 10 kufuata huduma ya matibabu katika kituo cha afya Murangi," anasema.

Anaongeza kuwa, hata wakazi wa vijiji vya Kata ya Bugwema, nao wana changamoto ya kutembea umbali kilomita 22, kufuata huduma ya afya katika zahanati ya Kijiji cha Masinono.

"Huo ni mfano mdogo wa jinsi wananchi wangu wanahangaika kutafuta huduma ya afya. Hii imenisukuma kuwahamasisha katika ujenzi wa zahanati, tukishirikiana na halmashauri yetu na wadau wengine wakiwamo wazawa wanaoishi nje ya jimbo," anasema.

Anasema anakazania ujenzi wa zahanati na vituo vya afya kwa vile anatambua kuwa mtu mwenye afya bora anaweza kufanya kazi vizuri na kujiletea maendeleo binafsi na taifa kwa ujumla.

Profesa Muhongo anasema, una vijiji vingi, ambavyo havijaanza kujenga zahanati, kwa vile zilianzia kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa kwanza na kisha baadaye vitageukia huko.

"Mimi niko bega kwa bega na wananchi wangu. Nimekuwa nikichangia kutoa saruji, mabati au kile ambacho kinafaa kulingana na mahitaji ya eneo husika, ili kufanikisha ujenzi huo wa zahanati na vituo vya afya," anasema.

Anaongeza kuwa mchango mwingine ambao amewahi kuutoa katika sekta ya afya ni magari matano ya wagonjwa, ambayo huwachukua wagonjwa na kuwawahisha kwenye matibabu.

Anasema kuwa mwaka juzi alipeleka madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali kutoka China kwenda jimboni mwake kwa ajili ya kutoa huduma ya afya bure kwenye baadhi ya vijiji ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuboresha afya za wakazi wa Musoma Vijijini.

Ujenzi unavyofanikishwa

Anasema kuwa, wananchi wamekuwa wakijitolea kusomba mawe, maji, mchanga huku wadau wengine wakiwamo wazawa wanaoishi nje ya jimbo hilo nao wakiwa mstari wa mbele kutoa chochote, ili kufanikisha ujenzi wa zahanati na vituo vya afya.

"Halmashauri ya Musoma Vijijini inasimamia kazi hiyo, huku wasaidizi wangu nao wamekuwa wakipita vijiji mbalimbali kuhamasisha wananchi umuhimu wa kuchangia ujenzi wa zanahati ili kusogeza huduma ya afya karibu yao," anasema.

Anafafanua kuwa, wasaidizi wake watatu amewagawia kila mmoja vijiji vyake ambavyo anatembelea kila siku ili kufuatilia shughuli mbalimbali za maendeleo na kupokea changamoto zinazowakabili wananchi.

"Kwa mfano, Fedison Massawa, anazungukia vijiji vya Tereguka, Mayani, Kataryo, Kiriba, Bwai Kwitururu, Bwai Kumusoma, Kurwaki, Mugango, Ngang'oma, Kwibara, Etaro, Busamba na Mmahare," anasema

Anavijata vijiji vingine vya msaidizi wake huyo kuwa ni; Nyakatende, Kamguruki, Kakisheri, Kigera Etuma, Kurukerege, Nyegina, Mkirira, KIemba, Kabegi na Nyasaungu.

Msaidizi wangu mwingine ni Verediana Mgoma ambaye anazungukia vijiji vya Bukima, Butata, Busungu, Bwasi, Makojo, Chitare, Murangi, Lyasembe, Kastamu, Kwikerege, Busekera, Bujaga, Kome, Buraga, Buira, Bukumi na Bugunda," anasema.
Prof. Muhongo anaendelea kuvitaja vijiji vingine vya msaidizi wake huyo kuwa ni  Chimati, Rusoli,  Musanja, Mabui Merafulu, Nyabaengere, Bulinga na Buanga.
"Msadizi wangu mwingine ni Hamisa gamba ambaye azungukia vijiji vya Saragana, Nyambono, Kandrema, Bugoji, Kaburabura, Muhoji, Masinono, Bugwema, Kinyang'erere, Suguti, Kusenyi, Wanyerere, Chirorwe, Chumwi, Seka, Kasoma, Kaboni, Mikuyu, Maneke, Kwikuba na Mwiringo...msimamizi wao wa jumla ni James Francis," anasema.

Anasema kuwa kwa utaratibu huo amekuwa karibu na wananchi na kusimamia vizuri ujenzi wa zahanati na vituo vya afya unaoendelea na pia kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.

"Kwa utaratibu huu ambao tumejiwekea ni kwamba hata kama mimi nina majukumu mengine ya kibunge, kazi zinaendelea kama kawaida jimboni kwa ajili ya maendeleo," anasema.
MaoniMaoni Yako