Mabao matano makali ya Okwi


HAKUNA ubishi tena, Emmanuel Okwi yupo mbioni kabisa kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara. Mabao yake 20 yanamuweka mbali na mastaa wengine wanaoweza kumfikia.
Ni jambo gumu kwa John Bocco mwenye mabao 14 na Marcel Kaheza mwenye 13 kumfikia Okwi. Ni jambo gumu zaidi hasa ikizingatiwa kuwa mechi zilizosalia ni mbili tu.
Endapo Yanga ingekuwa imara kama mwanzo halafu Obrey Chirwa mwenye mabao 12 angekuwa moto kama mwanzo, huenda tungeweka akiba ya maneno. Lakini kwa sasa ni jambo gumu kwa staa yeyote wa Ligi Kuu kumfikia Okwi. Kinachosubiriwa kwa sasa ni kuona Okwi atatwaa tuzo hiyo akiwa na mabao mangapi.
Pamoja na hayo, je umewahi kujiuliza yapi ni mabao makali zaidi ya Okwi msimu huu? Makala hii imeorodhesha mabao saba ya kusisimua zaidi ya staa huyo wa zamani wa Yanga, SC Villa ya Uganda, Sondersjke ya Denmark na Etoile Du Saleh ya Tunisia.
5. Simba vs Mtibwa
Okwi ameifunga Mtibwa Sugar mabao mawili msimu huu katika raundi zote mbili walizokutana. Aliwafunga ile ya mzunguko wa kwanza pale Uwanja wa Uhuru na mzunguko wa pili ambayo ilipigwa pale uwanja wa Jamuhuri na kumalizika kwa Simba kushinda 1-0.
Bao la mechi ya mzunguko wa kwanza ambayo ilichezwa Oktoba 15, lilikuwa tamu zaidi. Okwi alifunga goli hilo kwa njia ya faulo dakika ya 90+5, nje ya kidogo ya eneo la hatari baada ya beki Erasto Nyoni kuchezewa rafu na Ally Makalani wa Mtibwa Sugar. Okwi aliupiga mpira huo kwa shuti la mzungusho lililomshinda kipa Benedict Tinocco ambaye ndiye alikuwa nyota wa mchezo huo.
4. Simba vs Mbeya City
Katika mechi ya mzunguko wa pili ambayo ilichezwa Aprili 12, Simba iliifunga Mbeya City mabao 3-1, na utamu zaidi lile bao la kwanza ambalo alifunga Okwi katika dakika ya 16, mara baada ya piga nikupige kutokea langoni mwa Mbeya.
Okwi alikutana na shuti kali ambalo lilipigwa na Bocco ambalo lilipanguliwa na kipa wa Mbeya City Owen Chaima na kumpiga chenga ya mwili beki alikuwa anakuja kumzuia kwa mbele na kugeuza mpira katika mguu wa kushoto na kupiga shuti la chini chini lililoingia nyavuni.
Bao hilo lilikuwa tamu zaidi kutokana na chenga ya mwili ambayo Okwi alimpiga beki huyo huku shuti lake la likishindwa kuokelewa na Chaima na mabeki waliokuwa wamejaa langoni mwa Mbeya City.
3. Simba vs Mwadui
Katika mechi mbili za msimu huu ambazo Okwi amekutana na kikosi cha Mwadui ameweza kuwafunga magoli matatu. Aliwafunga mawili kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza na mzunguko wa pili moja. Mechi hii ya mzunguko wa kwanza ambayo ilichezwa Uwanja wa Uhuru Septemba 17, alizaa magoli makali mawili ambayo yote alifunga Okwi.
Bao la kwanza alifunga dakika ya saba mara baada ya kupokea pasi safi ya Shiza Kichuya nje ya boksi na kuuchota mpira uliomgonga beki na kutinga nyavuni.
Bao lingine alifunga dakika ya 67, mara baada ya kupokea pasi ya Mzamiru Yassin nje kidogo ya eneo la hatari na kumpiga chenga ya kumtisha kama anapiga shuti na mguuu wa kulia beki wa Mwadui akajitengea mguu wa kushoto na anapiga shuti kali lililokwenda moja kwa moja wavuni.
2. Simba vs Singida United
Simba mara baada ya kurejea katika Kombe la Mapinduzi Zanzibar ambalo walishindwa kufanya vizuri kwa kutolewa kwenye hatua ya makundi walikutana na timu bora kabisa, Singida United na kushinda mabao 4-0.
Katika mechi hiyo iliyochezwa uwanja wa Taifa Januari 18, mabao mawili kati ya hayo alifunga Okwi ambaye alikuwa ametokea benchi.
Bao murua zaidi ni lile la dakika 75, mara baada ya Okwi kuingia alipokea pasi kutoka kwa Said Ndemla katikati ya uwanja na alikimbia na mpira huo huku akiwa chini ya ulinzi wa beki Kennedy Juma ambaye aliweza kumpiga chenga na kupiga shuti lililotinga nyavuni.
1. Simba vs Ndanda FC
Simba ikiwa bado ina ujoto joto wa kuifunga Yanga, wiki moja baadaye ilikutana na Ndanda pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ndanda wanaopambana kuepuka janga la kushuka daraja walikaza kinoma. Bahati mbaya kwao ilikuwa kipindi cha pili, Okwi alipopokea mpira akiwa mbele kidogo ya katikati mwa uwanja na kutembea kwa kasi akikokota mpira huo kuelekea lango la Ndanda.
Mabeki wa Ndanda walishindwa kufahamu wafanye nini jambo lililotoa upenyo wa Okwi aliyewapindua na kubadilisha mpira kwenda mguu wa kushoto kisha kukunjuka shuti kali nje kidogo ya eneo la hatari ambalo lilimshinda kipa Jeremiah Kisubi na kwenda moja kwa moja wavuni.
Credit: Mwanaspoti
MaoniMaoni Yako