LECHANTRE afichua Siri ya Ubingwa Simba


KOCHA Mkuu wa Simba, Mfaransa, Pierre Lechantre, amesema haikuwa rahisi kwao kuuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara huku akiitaja siri kubwa ni kila mtu alitimiza majukumu yake ya ndani na nje ya uwanja.

Simba ilitangazwa kuwa bingwa kabla hata haijaifunga Singida United bao 1-0 kwenye Uwanja wa Namfua, juzi.
Kwa matokeo hayo, Simba imefanikiwa kufikisha pointi 68 katika msimu huu wa ligi huku wakiweka rekodi ya kutofungwa huku wakibakisha michezo miwili pekee.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Lechantre alisema walipitia changamoto nyingi ambazo walifanikiwa kuzivuka na kufanikiwa kuchukua ubingwa huo ambao waliutafuta kwa miaka mitano mfululizo.

Lechantre alisema, anawapongeza wachezaji, viongozi na benchi lake la ufundi kwa kufanya kazi pamoja na kushirikiana na kufanikisha malengo yao huku wakijipanga kwa ajili ya msimu ujao.
“Ninaamini kila Mwanasimba hivi sasa ana furaha kubwa moyoni mwake.

“Ni ukweli usiopingika kuwa ligi msimu huu ilikuwa na ushindani mkubwa kutokana na kila timu kupambana kuuchukua ubingwa, lakini niwapongeze wachezaji wangu kwa kupambana kufikia kuuchukua ubingwa huu.

“Kwa kweli tulionyesha mshikamano mkubwa hadi kufikia hatua hii, na nina furaha kutimiza ahadi yangu ya kuuchukua ubingwa huu kwani ni moja ya ahadi zangu nilizoahidi kabla ya kusaini mkataba Simba,” alisema Lechantre.

MaoniMaoni Yako