Tuesday, May 1, 2018

Kwasi asimulia mkasa wa Yondani

Tags


KIRAKA wa Simba, Mghana Asante Kwasi, amesimulia namna alivyokutana na sakata la kutemewa mate na beki wa Yanga, Kelvin Yondani ‘Vidic’.
Kwasi ambaye alicheza kwa kiwango cha juu juzi Jumapili wakati Simba ikiichapa Yanga bao 1-0 na kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikifikisha pointi 62, alisema tukio hilo lililenga kumtoa mchezoni.
“Kwanza aliniumiza mguu, nikamwambia mbona unaniumiza, baada ya hapo akaniambia acha maneno nitakutoa nje au unabisha, nikamwambia huwezi kunitoa kwani nimefanya nini, ndiyo akanitemea yale mate,” alisema Kwasi aliyewahi kutamba na Mbao FC na Lipuli kabla ya kutua Msimbazi.
Baada ya Kwasi kutemewa mate hayo, alienda kuripoti jambo hilo kwa mwamuzi, Emmanuel Mwandembwa, ambaye hata hivyo hakutoa uamuzi wowote.
“Nilijua ni mbinu tu za kutafuta ushindi, alitaka kunipandisha hasira ili nihamaki kufanya fujo ili nionyeshwe kadi au kunivuruga kisaikolojia, niliigundua janja yake na nikaamua kutuliza akili na kuupiga mpira,” alisema.
Chanzo: Mwanaspoti