Kuna tatizo Simba? Ujumbe tata wa manara wazua hofu na sintofahamu

Na George Mganga

Afisa Habari wa klabu ya Simba, Haji Manara, amezua utata kwa wadau na mashabiki wa timu hiyo kufuatia ujumbe wenye mafumbo aliouandika kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mbali na kuandika kwa ujumbe huo, Manara vilevile amejiondoka kwenye makundi mengi yaliyo katika mtandao wa WhatsApp huku sababu zikiwa hazijulikani.

Taarifa za chini ya kapeti ambazo si rasmi zinaeleza yawezekana kukawa kuna masuala hayajakaa sawa baina yake na uongozi wa juu mpaka kuelekea kujitoka kwenye makundi hayo na kuandika ujumbe huo wenye utata.

"Nia yangu ni njema sana ila mimi pia inna nyongo, sihitaji heshima ila walau nipewe utu ninaostahili, nimefanya kwa kadri nilivyojaaliwa na Mungu ila lazima tusonge mbele kwa maslahi mapana ya klabu" ameandika Manara kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Ujumbe umekuwa ni mgumu kutafsirika na mpaka sasa umewaweka wadau midomo wazi kwa kushindwa kuelewa Manara anamaanisha nini.

Salehjembe imefanya jitihahada za kumtafuta Manara ili aweze kulitolea ufafanuzi kauli hiyo lakini simu yake imekuwa haipatikani hewani.

MaoniMaoni Yako