Kocha Lachantre hataki utani Simba

SIMBA wanaendelea na mazoezi ya kujiwinda na mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Ndanda ambayo itapigwa Jumapili na kama wakipata pointi tatu watabakisha pointi moja tu ili kuwa mabingwa.
Kocha Mfaransa wa Simba Pierre Lechantre katika mazoezi waliyofanya juzi Jumatano katika Uwanja wa Uhuru, alionekana kuwa mkali na kuwakemea nyota wake waliokuwa wanazingua. Pierre ameliambia Mwanaspoti kwa mara ya kwanza kuwa wachezaji wake wameshaanza kuleta mzaha na kuona tayari wameshachukua ubingwa, baada ya ushindi wa mechi na Yanga kumbe si hivyo.
“Nimewaona wanafanya mazoezi kwa utaratibu na kujiaona wamemaliza na washabeba ubingwa baada ya kuichapa Yanga, mambo bado kabisa na hakuna muda wa kufanya mzaha. Tunatakiwa kushinda mechi mbili zaidi,” alisema.
“Nimewaambia sitaki kuona pasi za visigino wala madoido uwanjani, nawaona tu wanaacha kufanya mazoezi kwa nguvu. Nitakuwa mkali zaidi,” alisema Lechantre wakati kikosi chake kilipofanya mazoezi kwa saa mbili.
OKWI AZUA HOFU
Hata hivyo, straika Emmanuel Okwi hakuwepo katika mazoezi hayo na taarifa zilidai kuwa anasumbuliwa na maumivu ya kidole. Lechantre alisema katika mechi na Yanga Okwi alijitonesha amepewa mapumziko ya siku moja zaidi ili kuona kama anaweza kujiunga na wenzake ama kupumzika zaidi.
Chanzo: Mwanaspoti