Kipigo Cha Yanga Chamrudisha Lwandamina Yanga kiaina

KOCHA Mkuu wa zamani wa Yanga, George Lwandamina alirejea kwao Zambia na sasa anainoa Zesco United, lakini asikwambie mtu kipigo cha bao 1-0 ilichopewa Yanga na watani zao Simba Jumapili iliyopita kimerejesha kimtindo Mzambia huyo.
Lwandamina kumbe alikuwa akilifuatilia pambano hilo na kushuhudia Yanga ilala bao 1-0, licha ya kuwabana vilivyo wapinzani wao na kushindwa kujizuia kwa kuwapa pole vijana wake wa zamani akiwataka wapambane.
Mzambia huyo aliyetimka kwao baada ya kutofautiana na uongozi wa timu hiyo na tatizo kubwa likiwa kwenye maslahi akaamua kurudi timu yake ya zamani ya Zesco, alisema matokeo waliyoyapa Yanga ni sehemu ya mchezo.
Hata hivyo, aliwataka wachezaji wa Jangwani kupambana zaidi ili wafanikishe malengo yao mengine hasa katika ubingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
“Nimeona Yanga wamefungwa na Simba ni hali ya mchezo si mbaya, muhimu kwao ni kupambana ili kufanya vema zaidi katika mechi za kimataifa, kazi iliyopo mbele yao ni kubwa kuliko walikotoka,” alisema Lwandamina.
Lwandamina, ambaye hajawahi kupata ushindi mbele ya Simba tangu alipokuwa Yanga alizungumzia maisha yake Zesco na kudai hayamsumbui kwa sababu kwake si mapya amekuwa akiishi na kufanya kazi hapo kwa muda mrefu.
“Hapa hakuna jipya kwa sababu ni mahali ambapo nimeishi hapa kwa kipindi kirefu, ni maisha ambayo nayajua hivyo hakuna kinachonisumbua,” alisema Lwandamina.

Source Mwanaspoti
MaoniMaoni Yako