Kinachomng'oa Pluijm Singida United hiki hapa


Michuano ya Ligi Kuu Tanzania bara imemalizika wiki hii, huku kikosi cha Singida United ikishikilia nafasi ya tano Kati ya timu 16 zilizoshiriki ligi hiyo msimu huu.
  Singida imemaliza nafasi ya tano baada ya kuzidiwa ufundi na timu za Wekundu wa Msimbazi Simba waliotwaa Ubingwa wakiwapokonya watani zao Yanga walioishia nafasi ya tatu ikiiachia Azam FC nafasi ya pili huku ya nafasi ya nne ikichukuliwa na Tanzania Prisons.
Hata hivyo baada ya  Simba kutwaa ubingwa na Azam kusimama nafasi ya pili, imebainika kuwa ndio chanzo  kinachomng'oa Kocha Hans  Pluijm katika kandarasi yake kwenye kambi ya timu ya Singida United kutokana na mkataba wake kumtaka kuwa miongoni mwa nafasi hizo.
 Kocha Pluijm alisaini  mkataba wa kuinoa miaka miwili Singida United kwa msimu wa mwaka 2016/2017 na 2017/2018 baada ya kupanda Ligi Kuu harakati iliyowezeshwa na Kocha Felex Minziro lakini baadaye aliondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Mholanzi huyo.
 Kwa mujibu wa taarifa za ndani za klabu hiyo ya Singida United zinasema kuwa, kocha huyo analazimika kuondoshwa na kuletwa  mwingine baada ya kushindwa kutekeleza baadhi ya vipengele vilivyoko kwenye mkataba wake ikiwemo kutwaa ubingwa au kumaliza VPL  au nafasi ya pili.
 "Huyu Kocha alisaini mkataba unaomtaka ahakikishe kandarasi yake inalenga timu kutwaa ubingwa au hata kumaliza nafasi ya pili, lakini mara tu baada ya Simba kuchukua ubingwa alitakiwa kujitathmini katika nafasi yake maana zote ameshindwa hivyo kwa sasa tunamsubiri amalize fainali ya FA aondoke," kilisema chanzo hicho.
Aliongeza kuwa endapo matarajio ya walima alizeti hao yangefanikiwa walikuwa tiyari kumuongezea mkataba mnono Kocha Pluijm na kufanya usajili wa mapema chini ya ukocha wake kulinda nafasi yao lakini imeshindikana.
   Kwa upande wake, Kocha Pluijm alipoulizwa juu ya mkataba wake wa Singida na anautazamaje mkataba mpya unaodaiwa kusaini na Azam, alisema kuwa hawezi kuzungumzia swala la mikataba kwa sasa Bali anaelekeza nguvu zake katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam wanaotarajia kucheza na Mtibwa Juni 2 katika Uwanja  wa Sheikh Amri Abeid Arusha
   "Suala la mikataba kwa sasa naenda wapi au natoka wapi siwezi kuzungumzia wakati nina kibarua kikubwa mbele yangu ya fainali ya FA, kikubwa tambueni ukocha ndio kazi yangu na popote naweza kuweka kambi" alisema Pluijm
   Mkurugenzi  wa Singida United, Festo Sanga amesema kuwa kwa sasa bado hawajatoa taarifa rasmi juu ya mustakabali wa Kocha wao  Hans Pluijm lakini wanatarajia kutoa tamko kwenye mkutano na waandishi wa habari utakaofanyika mapema baada ya mchezo wa fainali ya FA.
   "Hizo fununu zilizopo juu ya kocha wetu si taarifa rasmi ya klabu yetu na bado hatujatoa tamko lolote kama anaondoka au anabaki hivyo mashabiki na wapenzi wa Singida watulie tutatoa taarifa kwa waandishi baada ya fainali ya FA tunayocheza Jumamosi Arusha," alisema Sanga.
MaoniMaoni Yako