Kagera Sugar yaipa onyo Simba


Ushindi walioupata Kagera Sugar juzi dhidi ya Njombe Mji umeonekana kuwapa jeuri benchi la ufundi na kutamba kuwa wanajipanga sasa kuvunja rekodi kwa kuwafunga Simba katika mechi ijayo.
Timu hiyo ya mjini Bukoba ilifanikiwa kuilaza Njombe Mji kwa mabao 3-1, ambapo inatarajia kuwavaa vinara wa Ligi Kuu Simba, ambao hawajapoteza mechi yoyote, mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Mei 20.
Hadi sasa Kagera Sugar imekusanya pointi 31 na kujikita nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ambapo tayari imeshajihakikishia kubaki kwenye Ligi Kuu msimu ujao.
Kocha Msaidizi wa kikosi hicho, Ally Jangalu alitamba kuwa baada ya kupata pointi tatu kwenye mchezo uliopita sasa timu imetulia na sasa wanajiandaa kutibua rekodi ya Simba kwa kuifunga.
Alisema kuwa licha ya pointi walizonazo sasa kuwa si haba,lakini bado wanahitaji ushindi mwingine zaidi ili kumaliza ligi katika nafasi sita za juu na kwamba inawezekana.
“Kwanza hadi kufikia sasa tunashukuru Mungu,tulikuwa na hali ngumu, lakini kidogo timu imetulia na hapa tunajiandaa kuvunja rekodi ya kuwafunga Simba ambao hawajapoteza mchezo wowote,” alisema Jangalu.
Kocha huyo aliongeza kuwa haikuwa kazi rahisi kuifikisha timu hatua hiyo, kwani ilipoanzia ilikuwa ni ya kushuka daraja mapema, hivyo lazima wajipongeze.
Credit: Mwanaspoti
MaoniMaoni Yako