Friday, May 25, 2018

Jinsi Ya Kumtambua Mwanaume Tapeli Wa Mapenzi

TagsDUNIA ya sasa imejaa sarakasi nyingi za mapenzi. Kila mmoja analia na maumivu yake, hakuna aliye salama, maana siku hizi usaliti umegeuzwa kama ni fasheni.

Watu wanaishi kwa hofu. Hakuna kuaminiana tena, kila mtu ana kumbukumbu mbaya. Matokeo yake tunatengeneza kizazi cha kuishi bila kuaminiana. Tunatengeneza kizazi kisichoamini tena katika misingi ya ndoa. Kizazi kisichoishi katika maadili mazuri ya mke na mume, kulea familia na mambo mengineyo.

Bahati mbaya sana suala hili la uhusiano linahusisha mtu na moyo wake. Waswahili wanasema moyo wa mtu ni kama kichaka, huwezi kujua anawaza nini ndani ya moyo wake. Unaishi na mtu unamwamini kwamba mpo katika safari moja, kumbe mwenzako ana lake jambo. Anakuzuga tu kama anakupenda kumbe hakupendi.

Mawazo yake na akili yake bado iko safarini inatafuta mtu wa kumpenda. Lakini si ajabu pia kwamba, wakati akiwa na wewe, upande wa pili ana mwingine ambaye amewekeza kisawasawa penzi lake, anashindwa tu kukuambia ukweli.

Anajitahidi kukuficha usijue upande wake wa pili. Wakati wewe ukiamini upo na mtu sahihi kumbe mwenzako anakufanya wa ziada. Licha ya kuwa tatizo hili linawakumba watu wengi, lakini kimsingi wahanga wakubwa wa tatizo hili ni wanawake.

Kasumba ya wanaume kujihalalisha kwamba wao wanastahili kuwa na wanawake wengi ndiyo inayosababisha wanawake wengi wawe waathirika katika hili. Wanaume kwa tamaa zao wana nafasi kubwa ya kuwa matapeli wa mapenzi kuliko wanawake.
UTAMJUAJE MWANAUME TAPELI?
Licha ya kuwa na mbinu nyingi za udanganyifu lakini tapeli wa mapenzi unaweza kumbaini kuanzia hatua za awali pindi anapoanza kukuweka mikononi mwake. Msome anakuja kwa gia gani? Yawezekana akakuambia kuwa atakuoa lakini hilo usilitilie maana haraka; wewe weka akiba ya kumpenda.
Endelea kumfuatilia taratibu mwenendo yake. Angalia nafasi anayokupatia na jinsi anavyoheshimu hisia zako. Angalia papara zake katika kutekeleza matamanio ya mwili, utambaini tu kwamba anachokitaka kwako ni tendo tu na baada ya hapo hatokuhitaji tena. Usimpende mwanaume wa aina hiyo. Jipe muda wa kumchunguza. Muweke karibu ili upate
kumwelewa zaidi, mathalan waweza jenga desturi ya kukaa naye mara kwa mara huku nia yako ikiwa ni kumsoma zaidi mazungumzo yake, tabia na maisha yake kwa jumla. Mchunguze ujue je ni kweli ana nia ya dhati ya kuwa na wewe? Safari yake ya nyuma ikoje? Kwako ana matarajio gani? Nasisitiza usimpende katika hatua hizi, muweke karibu.
Tapeli huwa hawezi kuvumilia muda mrefu, hawezi kukuficha muda mrefu. Atataka mjuane, mmalizane haraka. Mwenye mapenzi ya dhati, atatengeneza mazingira ya urafiki mzito (strong relationship). Atajikita katika kukuweka karibu na marafiki zake, ndugu zake na hata wazazi wake.
Tapeli wa mapenzi hana muda wa kukutambulisha sana kwa jamaa zake kwa sababu anajua hana safari ndefu na wewe. Lakini mtu wa aina hii huwa ni msiri sana katika mambo yake hususan yale ya msingi na yenye tija katika mustakabali wa maisha. Tapeli hahitaji umjue sana, hataki uwajue ndugu zake wengi.
Tapeli huwa ni muongomuongo. Si mtu wa kukuweka wazi ratiba yake ya siku, kazi anayofanya na eneo alilopo hapendi ujue. Tapeli mara nyingi mnapokutana si mtu wa kuwa huru hata katika mawasiliano yake. Simu itafichwafichwa, akitaka kuiweka mezani ataigeuza nyuma mbele ili kuficha usione au kusikia ikiita.
Tapeli anaweza kukuficha mara moja mara mbili lakini hawezi kukuficha wakati wote. Utambaini tu ukijipa muda mzuri wa kumsoma! Ni matumaini yangu utakuwa umepata picha, tafakari na uchukukue hatua.
Credit: Global Publishers