Heshima kwa Simba Sc


MABINGWA wapya wa Ligi Kuu Bara, Simba leo Jumamosi watakuwa na kibarua kizito dhidi ya Singida United ambao wamepania kulipiza kisasi cha mechi ya kwanza waliyopoteza 4-0 jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, kwa Simba ni mechi ya heshima zaidi kwa kuwa tayari imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu, lakini kwa upande wa Singida United ni tofauti kabisa kwani, wanaingia wakiwa na mambo mawili. Kwanza, wanataka kumaliza ligi katika nafasi za juu, lakini pia wanataka kulipa kisasi kwa kupigwa 4G pale Taifa, Dar es Salaam.
Singida imefuzu fainali ya Kombe la FA hivyo imepanga kutumia mchezo dhidi ya Simba kama fursa ya kujiweka vizuri.
Lakini, Mwanaspoti limekuchambulia mambo muhimu ambayo yanaweza kutokea katika mchezo huo ambao, umevuta hisia za za mashabiki wengi.
SIMBA NA REKODI
Simba imeshatwaa taji la Ligi Kuu ililokuwa inalisaka kwa mwaka wa tano sasa, lakini katika mechi hii itakuwa inacheza kwa morali kama ilivyokuwa kwenye mechi nyingine ambazo imeshacheza.
Sababu inayowafanya nyota wa Simba kucheza kwa morali ni kutaka kulinda rekodi ya kuchukua ubingwa bila kufungwa msimu huu, kama walivyofanya mara ya mwisho alivyochukua ubingwa msimu wa 2009/10.
Kwa Simba kutofungwa hata mechi moja tangu kuanza kwa ligi msimu huu huku Singida United ikitaka kulipiza kisasi, ni dhahiri kuwa mechi hiyo itakuwa ngumu sana.
Singida walifanya mazoezi yao ya mwisho jana asubuhi kwenye Uwanja wa Namfua huku wachezaji wa timu hiyo wakionyesha morali ya hali ya juu kuliko kawaida.
Simba wao walifanya mazoezi yao ya mwisho kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma na mchana wa jana waliingia Singida huku wachezaji wake wakiwa na morali ya hali juu tena na furaha ya ubingwa ndani yake.
Hayo yote ni miongoni mwa viashiria kuwa mechi itakuwa na shoo za kibabe kwelikweli ingawa dakika 90 ndio zinaweza kubadilisha hali ya mechi kama ilivyotegemewa katika mechi ya mzunguko wa kwanza kuwa, itakuwa ngumu lakini mambo yakabadilika.
MECHI YA MABAO
Achana na magoli manne ambayo yalipatikana kwenye mechi yao ya mzunguko wa kwanza, mechi ya leo Jumamosi kunaweza kuwa na matokeo ya kufungana magoli mengi ambayo yatakuwa si chini ya mawili.
Kocha wa Singida Mdachi, Hans Van Pluijm kawaida yake ni kutumia mfumo ya kushambulia muda wote hasa katika mechi hii ambayo wanataka kuonyesha kuwa, ni miongoni mwa timu bora zilizoliwa nchini kwa sasa.
Vivyo hivyo kwa kocha wa Simba Mfaransa, Pierre Lechantre naye mara nyingi anapenda kutumia mfumo wa kushambulia japokuwa wakati mwingine huwa anajilinda sana.
Mashabiki kufurika
Mwanaspoti imeweka kambi hapa Singida tangu Alhamisi ambako, mashabiki wengi wa Simba wanamiminika mjini hapa kusherehekea ubingwa wao.
Mashabiki wa Singida hawakuwa nyuma walikuwa wakikatiza katika mitaa ya Singida wakitamba kuvunja rekodi ya Simba kutokufungwa na kulipa kisasi cha mechi ya kwanza.
Hali hiyo inafanya mechi ya leo kuweza kujaza mashabiki uwanjani Namfua kuliko nyingine yoyote ya ligi kuu ambayo imechezwa mjini hapa msimu huu.
Credit: Mwanaspoti
MaoniMaoni Yako