Hans Poppe huenda akafungwa jela maisha


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa amri dhidi ya washtakiwa wawili; Zacharia Hans Poppe na Franklin Lauwo, wakamatwe popote walipo.
Amri hiyo imetolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, baada ya Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, kubadilisha Hati ya Mashtaka na kuwaongeza watuhumiwa hao.
Swai alidai amewatafuta washtakiwa hao tangu mwezi Machi ili kuwaunganisha bila mafanikio na kuomba hati ya kuwakamata kwani hawakuwepo mahakamani.
Washtakiwa hao wameongezwa katika kesi ya utakatishaji fedha na kughushi inayomkabili Rais wa Simba, Evans Aveva na Makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’.
Katika shtaka la kwanza la kula njama, inadaiwa kati ya Machi 10 na 16, 2016 washtakiwa Aveva na Nyange kwa pamoja walikula njama na kutenda kosa.
Katika shtaka la pili ambalo ni matumizi mabaya ya madaraka, Aveva na Nyange katika tarehe hizo hizo wanadaiwa kuandaa nyaraka za kuhamisha dola za kimarekani 300,000 kutoka kwenye akaunti ya klabu ya Simba kwenda akaunti ya Aveva wakijua kuwa wanachofanya ni kosa.
Shtaka la tatu la kughushi linalowakabili Aveva na Nyange inadaiwa katika tarehe hizo hizo wakiwa Dar es Salaam kwa pamoja walighushi nyaraka ikionyesha Simba inalipa mkopo wa dola 300,000 kwa Aveva kitu ambacho si kweli.
Katika shtaka la nne la kuwasilisha nyaraka ya kughushi, inadaiwa Aveva Machi 15,2016 katika Benki ya CRDB aliwasilisha nyaraka ya uongo ikionyesha Simba inalipa mkopo wa dola 300,000.
Shtaka la tano ni utakatishaji fedha linalomkabili Aveva ambapo inadaiwa kati ya Machi 15,2016 katika benki ya Barclays Mikocheni alijipatia dola za kimarekani 187,817 wakati akijua zimetokana na kughushi.
Katika shtaka la sita la utakatishaji fedha, inadaiwa Nyange alimsaidia Aveva kujipapatia dola 187,817 kutoka kwenye akaunti ya Simba wakiwa wanajua fedha hizo zimetokana na zao la kughushi.
Shtaka la saba ambalo ni kughushi pia linalowakabili Aveva, Nyange na Poppe, kwa pamoja wanadaiwa walighushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28,2016 wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zina thamani ya dola 40,577 huku wakijua si kweli.
Katika shtaka la nane la kuwasilisha nyaraka ya uongo, Aveva anadaiwa kuwasilisha hati ya malipo ya kibiashara ya uongo kwa Levison Kasulwa ya Mei 28, 2016 kwa madhumuni ya kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya dola 40,577.
Shtaka la Tisa la kutoa maelezo ya uongo, ambapo inadaiwa Aveva, Nyange na Poppe, Machi 10,2016 na Septemba 30,2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya dola 40,577.
Katika shtaka la mwisho ni kuendesha biashara bila kufuata sheria, kati ya Machi na Septemba 2016, Lauwo akiendesha biashara kama mkandarasi kwa kujenga Uwanja wa Simba uliopo Bunju wakati akiwa hajasajiliwa.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa walikana na kupelekwa rumande kutokana na shtaka la utakatishaji linalowakabili kutokuwa na dhamana.
Wakili wa utetezi, Steven Mwakibolwa, aliiomba mahakama kuendeleza kesi kwa washtakiwa wawili waliopo, lakini hakimu Simba alieleza kuwa kwa kuwa kuna washtakiwa walioongezwa na wanatakiwa kukamatwa hivyo, hawataweza kuendelea hadi watakapokuwapo mahakamani.
Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Mei14, 2018 kwa ajili ya kutajwa.
Chanzo: Mwanaspoti
MaoniMaoni Yako