Fedha zaamua Ligi Kuu Bara


Dar es Salaam.Nguvu ya fedha imekuwa na uhusiano wa moja kwa moja na matokeo ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2017/2018.
Ligi hiyo ilimalizika juzi Jumatatu kwenye viwanja vinane tofauti huku Simba ikiwa tayari imetwaa ubingwa wa mashindano hayo.
Mafanikio au kushindwa kwa idadi kubwa ya timu zilizoshiriki ligi hiyo kumechangiwa na nguvu za kiuchumi zilizokuwa nazo katika msimu huu.
Tathmini iliyofanywa na gazeti hili imebaini timu zilizokuwa na bajeti iliyojitosheleza, zilifanya vizuri na zilizoyumba kiuchumi zilipata wakati mgumu na kusababisha Majimaji ya Songea na Njombe Mji kushuka daraja.
Simba iliyotwaa ubingwa na kumaliza unyonge wa kukaa misimu mitano mfululizo bila kupata taji la Ligi Kuu, ni kielelezo halisi cha nguvu ya fedha ilivyoamua matokeo na ubora wa timu msimu huu.
Ikiwa na jeuri ya fedha kutoka kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘MO’ na mafungu ya udhamini kutoka Kampuni za Azam Media, Sportpesa na Vodacom, Simba ilitenga Sh4.7 bilioni kama bajeti yake msimu huu.
Kiasi hicho cha fedha kilikuwa kikubwa kuliko bajeti ya klabu nyingine katika msimu huo ambacho kilitumika kwa usajili, mishahara, posho za timu, kulipia huduma za malazi, usafiri na matibabu.
Fungu hilo kubwa la bajeti liliibeba Simba ambayo katika usajili ilitumia Sh1.3 bilioni zilizoibuka na kikosi imara kwenye ligi ambacho kilitwaa ubingwa kikiwa na mechi tatu mkononi huku kikipoteza moja.
Simba ilifunga idadi kubwa ya mabao 69 na ndio timu iliyoruhusu kufungwa machache zaidi 15.
Wakati mambo yakiwaendea vizuri Simba, hali ilikuwa mbaya kwa Yanga ambayo ilijikuta ikiporomoka ghafla na kumaliza ligi kwenye nafasi ya tatu, matokeo yanayoonekana kuchangiwa na hali mbaya ya kiuchumi.
Yanga ambayo misimu mitatu iliyopita ilikuwa moto wa kuotea mbali, safari hii ilifanya vibaya baada ya kukabiliwa na mdororo wa kiuchumi uliochangia kwa kiasi kikubwa kujiondoa kwa aliyekuwa Mwenyekiti na mfadhili mkuu, Yusuf Manji.
Hali mbaya ya kiuchumi iliwafanya mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu wakiwa wametwaa mara 27, kuingia kwenye mgogoro wa mara kwa mara na wachezaji wake tegemeo.
Wachezaji waliweka mgomo baridi kushinikiza malipo na stahiki zao za mishahara, posho na fedha za usajili jambo ambalo lilichangia kushusha morali kwa wachezaji.
Mbali na hilo, timu hiyo ililazimika kusajili kundi kubwa la wachezaji vijana ambao wengi hawakuwa na uzoefu wa kutosha na walishindwa kuisaidia Yanga kupata matokeo mazuri katika mechi ngumu.
Azam iliyomaliza nafasi ya pili, pamoja na kikosi chake msimu huu kujaza idadi kubwa ya vijana, ilinufaika na nguvu ya fedha iliyonayo ambayo ilileta utulivu kwenye kikosi chao kutokana na wachezaji wake kupata huduma bora na stahiki kwa wakati.
Faida ya fedha pia imeonekana kwa Singida United ambayo pamoja na kuwa moja ya timu tatu zilizopanda Ligi Kuu, ilipambana kikamilifu na timu zenye uzoefu ambapo ilimaliza kwenye nafasi ya tano katika msimamo wa ligi.
Singida ilibebwa na fedha za udhamini kutoka Kampuni za Azam Media, Vodacom, Halotel, Maji ya Uhai, Yara na Sportpesa ambazo ziliipa jeuri ya kusajili nyota wa ndani na nje ya nchi ambao waliboresha kikosi cha timu hiyo.
Namna vile ambavyo ukata uliiathiri Yanga kwenye vita ya ubingwa, ndivyo ilivyotokea kwa timu tatu zilizoshika mkia kwenye ligi hiyo Majimaji, Ndanda na Njombe Mji.
Njombe Mji, Majimaji zilizoshuka daraja na Ndanda iliyoponea chupuchupu, zilionjeshwa joto ya jiwe na nguvu duni ya kiuchumi ambazo zilikuwa nazo tangu mwanzoni hadi mwishoni mwa ligi.
Timu hizo kwa nyakati tofauti zilijikuta zikipambana na migomo ya wachezaji waliokuwa wakishinikiza malipo ya stahiki zao.
Pia zilishindwa kusajili wachezaji bora ingawa walipata maandalizi mazuri mwanzoni na wakati msimu ulipokuwa unaendelea, jambo lililozifanya zigeuke wasindikizaji kwenye ligi msimu uliomalizika.
Kauli za wadau
Mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay alisema kuwa eneo la waamuzi linatakiwa kuboreshwa kwa kuwa baadhi yao walifanya makosa ya kujirudia mara kwa mara ambayo yalitia doa mashindano hayo.
“Adhabu ya kuwafungia sio suluhisho wakati tayari timu moja imeshaathirika na uamuzi mbovu waliofanya, hatukatai makosa ya kibinadamu yanakuwepo, lakini kuna waamuzi wanaona makosa ya upande mmoja tu na msimu huu wameonekana hivyo msimu ujao wasifumbiwe macho,” alisema Mayay, mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars.
Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali mstaafu, Idd Kipingu alisema Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), linatakiwa kutupia jicho waamuzi aliodai kuwa wanatakiwa kuchezesha ligi wanapaswa kuwa na uzoefu usiopungua miaka mitano.
MaoniMaoni Yako