Everton yaibua hamasa Simba kwenye Michuano ya SportPesa Cup

WAKATI simba leo ikicheza mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kiungo wa timu hiyo, Jonas Mkude, amesema mawazo yake yapo kwenye michuano ya SportPesa Super Cup  yatakayofanyika Nairobi kuanzia Juni 3, mwaka huu.
Mkude, ambaye yupo mjini Songea pamoja na kikosi cha Simba kwa ajili ya mchezo dhidi ya Majimaji, amesema wanautaka ubingwa wa SportPesa ili wapate nafasi ya kucheza na timu kubwa ya Everton ya England.
"Tunautaka ubingwa wa SportPesa na hilo ndilo tunaloliwazia,  kila mchezaji anataka kuona tunapata nafasi ya kucheza na Everton kwa kuchukua ubingwa wa michuano hii, " alisema Mkude.
Alisema kwenye michuano hiyo watafanya kama kile walichokifanya kwenye ligi msimu huu.
"Tunaomba tumalize ligi salama, lakini kazi yetu tunaihamishia Nairobi, moto utakuwa ule ule kama ilivyokuwa kwenye ligi," alisema.
Simba pamoja na Yanga, Singida United na JKU ya Zanzibar zitaiwakilisha nchi kwenye michuano hiyo itakayoshirikisha pia timu nne kutoka Kenya.
Bingwa wa michuano hiyo inayoandaliwa na Kampuni ya SportPesa, atakata tiketi ya kwenda England kucheza mchezo maalum na klabu ya Everton kwenye Uwanja wa Goodson Park nchini England.
Credit: IPP Media
MaoniMaoni Yako