Etienne sasa kumrithi Pluijm Singida United

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Mbao FC ya jijini Mwanza, Etienne Ndayiragije, anatarajiwa kutangazwa rasmi kuwa kocha mpya wa Singida United inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, imefahamika.

Ndayiragije anatua Singida United, kurithi mikoba itakayoachwa na Mholanzi, Hans van der Pluijm, ambaye tayari ameshaaga na anatarajiwa kujiunga na Azam FC ya jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Singida United, Festo Sanga, alisema mazungumzo na Ndayiragije yanaendelea vyema na mara baada ya kukamilika watampa mkataba.
Festo alisema wamefikia uamuzi wa kusaka kocha mpya baada ya Pluijm kueleza anataka kuondoka msimu wa ligi utakapomalizika.
"Pluijm anaondoka mwishoni mwa msimu, tunatakiwa kusaka kocha mpya, ila bado hatujampa mkataba Ndayiragije kama ambavyo inaelezwa," alisema kwa kifupi mkurugenzi huyo.
Alisema mchakato wa kusaka kocha mpya unafanyika kwa umakini zaidi kwa sababu wanahitaji kuwa na mwalimu ambaye ataweza kuisaidia timu na kuhakikisha wanapata mafanikio zaidi katika msimu ujao.
Hata hivyo, tayari Pluijm na kikosi cha kwanza cha timu hiyo kimeshafika jijini Arusha tangu juzi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Mtibwa Sugar ambao utapigwa Juni 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Bingwa wa michuano hiyo ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hapo mwakani.
Credit: IPP Media
MaoniMaoni Yako