Cristiano Ronaldo Jr atakuwa stadi wa kandanda kama babake?
Mwana wa mhunzi asiposana hufukuta na katika ulingo wa kandanda, baadhi ya wana wa wachezaji soka hodari wamefanikiwa kuwaiga wazazi wao.

Lakini je, mwana wa mshambuliaji nyota wa Real Madrid Cristiano Ronaldo atafanikiwa katika hili?

Ronaldo amekuwa mfungaji mabao hodari na kujizolea sifa si haba.

Mreno huyo mwenye miaka 33 amekuwa akifunga kwa wastani mabao 50 kila msimu katika misimu tisa ambayo amekuwa Real Madrid.

Lakini miaka inavyosonga ndivyo anavyokaribia kufikisha umri wake wa kustaafu.

Watu wameanza kufikiria jinsi ulimwengu wa soka utakavyokuwa bila ufungaji mabao wa Ronaldo na ushindani wake mkali na Lionel Messi anayechezea Barcelona.

Mambo yakienda vyema hata hivyo, dalili zinaonesha pengine watu hawatakaa muda mrefu bila kuwa na Ronmaldo mwingine kwenye soka.

Ronaldo ameonekana katika kila hatua kumuandaa mwanawe wa kiume Cristiano Jr kuwa mchezaji soka mahiri na pia kuzoea maisha ya umaarufu na kuangaziwa kila wakati na wanahabari.

Mtoto huyo ana miaka saba pekee lakini ameonesha baadhi ya ustadi wa babake.

unaweza kumuona akiwachenga mabeki na kisha kufunga wakati wa mapumziko debi ya Madrid uwanja wa Bernabeu ukiwa umejaa mashabiki.

Hapa, alipigwa picha akijaribu kuigiza bao maarufu la 'bicycle-kick' ambalo babake alifunga dhidi ya Juventus ya Italia wakati wa mechi ya robofainali Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Picha inaonekana hakufanikiwa hasa, lakini inaonekana kuna matumaini katika juhudi za Cristiano Ronaldo Sr kujaribu kumfunza mwanawe ustadi wa kufunga mabao.

Kufikia sasa, Cristiano Jr tayari amepata baadhi ya ujuzi na ustadi wa babake wa ufungaji mabao.

Hapa chini, tunaangazia baadhi ya mambo mengine ambayo mwana amefunzwa na babake, akarithi au kuiga.

Kufanya mazoezi makali

Cristiano Jr kawaida huenda kwenye 'gym' kwa mazoezi makali akiandamana na babake.

"Daddy, nitakuwa kama wewe," Ronaldo anaandika kwenye ujumbe ulioandamana na picha moja aliyopakia kwenye Instagram akionesha misuli ya mwanawe iliyotuna.

Mtoto huyo anaonekana kuwa na misuli ambayo bila shaka ni matokeo ya mazoezi hayo na pengine vinasaba vya babake.

Ufungaji penalti.

Ronaldo baba amekuwa stadi sana wa kufunga mikwaju ya penalti ambapo amefunga zaidi ya penalty 100 katika maisha yake ya uchezaji.

Si ajabu kwamba amemfunza mwanawe kufunga mikwaju hiyo.

"Ukishindwa kufunga utalazimika kufanya 'push-ups' 10," Ronaldo anasema, kabla ya kumpa mwanawe mpira ajaribu mara tatu kufunga.

Junior alichukua fursa hiyo, ya kwanza akakosa na pili akagonga mwamba wa goli. Lakini jaribio la tatu akafunga.

"Lakini nimefunga," Cristiano Jr anasema kabla ya Ronaldo kumwambia: "Zifanye hata hivyo [push-ups]. Si kitu, ni 10 pekee."

Junior amefunza hata kusherehekea baada ya kufunga mabao, ingawa hamfikii babake kusema kweli.

Kupiga selfie.

Iwapo huwa unamfuatilia sana Ronaldo mitandao ya kijamii, utagundua kwamba yeye ni stadi wa kujipiga picha. Mwanawe hayuko mbali pia. 

Faida gani ufanye mazoezi na kuujenga vyema mwili kisha usiwaoneshe wengine na kuringa?

Unaiona tofauti hapa?

Mtindo.

Wachezaji soka huhitajika kuonyesha hadhi na haiba yao nzuri kwa mavazi na mitindo ndani na nje ya uwanja. Ndio maana huonekana wakiwa na mavazi ghali na magari ya kifahari.

Cristiano Jr anafahamu hilo bila shaka, anajua mtu anavyohisi akiwa ndani ya gari la thamani ya £2.15m.

Na tayari anajua kuigiza mitindo ya mavazi, ambapo ameonekana mtanashati akipigwa picha za mauzo ya mavazi akiwa na babake.

Lakini baada ya yote, atahitaji kujizolea umaarufu wake uwanjani, na kushinda tuzo ya Ballon d'Or mara tano, na kuwa na sanamu kadha zake katika miji mbalimbali ndipo aweze kumfikia babake.

Lakini bado ana miaka mingi ya kufanya hivyo. 
Chanzo: BBC


MaoniMaoni Yako