Azam yapania ya pili ikiivaa Yanga

NAODHA wa Azam FC, Himid Mao, amesema wana kila sababu ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Bara, inayomalizika leo.

Himid, alisema hayo jana na kusisitiza watapambana kwenye mchezo wa leo dhidi ya Yanga utakaochezwa usiku kwenye Uwanja wa Taifa.
Alisema kwao kama wachezaji mchezo wa kesho una umuhimu mkubwa sana na kama watafanikiwa kushinda itakuwa furaha kwao.
"Yanga walitufunga kwenye mchezo wa kwanza, mchezo huu umekuja tukiwa tunahitaji kushika nafasi ya pili kwenye msimamo, lakini pia tunataka kulipiza kisasi cha kufungwa kwenye mchezo wa kwanza, " alisema Himid.
Yanga ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Azam  Complex.
"Hatutawadharau Yanga kwa sababu wamekuwa na matokeo yasiyo mazuri siku za karibuni, tutaingia kwa tahadhari, "alisema Himid.
Azam wanahitaji sare au ushindi ili kumaliza nafasi ya pili nyuma ya Simba ambao tayari wameshatwaa ubingwa, wakati Yanga yenyewe inahitaji ushindi ili kuweza kumaliza ligi nyuma ya Simba.
Credit: IPP Media
MaoniMaoni Yako