Azam yajivunia vijana, sasa kusajili 'majembe'


AZAM imefanikiwa kumaliza ligi kwenye nafasi ya pili na viongozi wa timu hiyo wamewapongeza wachezaji wao ambao awali hawakupewa nafasi ya kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri msimu huu, huku klabu hiyo ikiahidi kushusha majembe ya hatari dirisha hili la usajili.

Kabla ya kuanza msimu huu, Azam iliachana na wachezaji wake sita wa kikosi cha kwanza kwa kile kilichoelezwa sera mpya ya klabu hiyo ya kutaka kubana matumizi.
Wachezaji walioondoka na kujiunga na timu nyingine ni pamoja na John Bocco, Aishi Manula, Shomari Kapombe , Erasto Nyoni pamoja na Gadiel Michael.
Hata hivyo, huku ikiwatumia wachezaji wake vijana, Azam imefanikiwa kumaliza ligi ikiwa nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Simba.
Nafasi hiyo walijihakikishia baada ya juzi usiku kumaliza ligi kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Yanga.
Akizungumza na Nipashe, Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Abdulkarim Amin 'Popati', alisema wanajivunia wachezaji wao waliopambana tangu kuanza kwa ligi mpaka kumalizika.
"Baada ya kuondoka kwa baadhi ya wachezaji wetu, tulitumia zaidi vijana, pamoja na kuwa hawakuwa na uzoefu kwenye ligi, wameipeleka Azam mpaka nafasi ya pili tofauti na matarajio ya wengi," alisema Abdulkarim.
Alisema kwa sasa wameanza kukisuka upya kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao wa ligi huku wakianza kwa kumsajili mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma.
Alisema wapo wachezaji wengine wanaofanya nao mazungumzo ndani na nje ya nchi na pindi mambo yakikamilika watatoa taarifa.
MaoniMaoni Yako