Azam FC, Yanga Kugombania nafasi ya pili

AZAM FC tayari imeingia kambini kujiandaa na mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu Tanzania Bara, na timu hiyo imewatahadharisha wapinzani wao Yanga kujiandaa kupokea kipigo kwa sababu wanataka kumaliza nafasi ya pili.


Msemaji wa klabu hiyo, Jaffar Iddi, amesema lengo la kuingia kambini ni kuhakikisha wanamaliza Ligi Kuu msimu huu wa 2017/18 kwa kasi na kwa kupata ushindi katika mechi hiyo ya kufunga pazia.
Iddi alisema wanaiheshimu Yanga lakini lengo lao ni kuhakikisha wanamaliza ligi wakivuna pointi tatu na kukusanya nguvu kwa ajili ya msimu ujao.
"Timu yetu tayari ipo kambini kwenye hosteli zetu, kikubwa lengo letu ni kuona tunamaliza ligi kwa ushindi, tunacheza na Yanga siku ya Jumatatu lakini kabla ya kuvaana na sisi wenzetu wanamchezo mwingine (dhidi ya Ruvu)," alisema kiongozi huyo.
Mchezo huo wa Jumatatu utatoa picha kamili ya timu gani itamaliza ligi kwenye nafasi ya pili nyuma ya Simba,
Azam mpaka sasa wameishikilia nafasi hiyo kwa kuwa na pointi 55 huku Yanga wakiwa nafasi ya tatu kwa pointi 51 huku ikiwa na michezo miwili mkononi.
Lakini kama Yanga itapoteza mchezo wa kesho dhidi ya Ruvu Shooting, Azam itajihakikishia nafasi ya pili hata kama itafungwa kwenye mchezo huo wa mwisho dhidi ya mabingwa hao wa zamani.
 Credit: IPP Media
MaoniMaoni Yako