Alikiba aeleza kwa nini alimgeuzia mkono DiamondDar es Salaam. Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Alikiba amefunguka kuhusu namna alivyosalimiana na msanii mwenzake, Nassib Abdul au Diamond kwa kumgeuzia mkono walipokutana katika msiba wa Masogange kwenye viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam.


Wawili hao walipokutana, Alikiba badala ya kumpa kiganja cha mkono kama ilivyozoeleka, alimpa mkono kwa kuugeuza jambo ambalo liliibua mjadala katika mitandao mbalimbali ya kijamii.


Akizungumza leo Ijumaa Mei 11, 2018 katika kipindi cha 360 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Clouds, ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipofunga ndoa Aprili 19, 2018, Alikiba amesema usalimiaji ule ndio wanaotumia wanaume kusalimiana na hakuna kitu kingine.


“Unajua wanaume tuna staili zetu za kusalimiana ambazo ni tofauti kabisa. Hakukuwa na kingine kama ambavyo watu walijadili kwenye mitandao ya kijamii,” amesema.


Alipoulizwa kuhusu sababu ya yeye kuondoka muda mfupi baada ya Diamond kuwasili katika viwanja hivyo, amesema ilitokana na kuwa katika fungate ya harusi yake, hivyo ingekuwa ngumu kukaa muda mrefu eneo hilo.


“Unajua hata kwenda nilifanya kuomba ruhusa kwa mke wangu ili nishiriki katika tukio hilo ambalo kidini pia ni ibada na nilipomaliza kilichonipeleka nikaondoka,” amesema Kiba ambaye kwa sasa anatamba na kibao cha Seduce Me.
Credit: Mwananchi
MaoniMaoni Yako