Yanga kuhama nchi


HABARI ndio hiyo, mabosi wa Yanga wametuma salamu mtaa wa pili. Yanga inautaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu ili kuendelea kuwa wababe dhidi ya mahasimu wao, Simba.
Iko hivi. Yanga leo Jumapili wanashuka dimbani pale Namfua kupepetana na Singida United, katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la FA.
Lakini, hiyo mechi na Singida United sio ishu kubwa kabisa na kama vipi achana nayo isikuumize kichwa. Yanga ikimaliza mchezo huo itarejea jijini Dar es Salaam, kuwasubiri Welaytta Dicha ya Ethiopia kwa mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano kuwania kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Unaambiwa baada ya hapo, vijana wa George Lwandamina watakula mwewe hadi Addis Ababa, Ethiopia kwa mechi ya marudiano dhidi ya wababe hao wa Sodo.
Utamu uko hapa sasa, mabosi wa Yanga wamepiga hesabu kali kwelikweli jinsi ya kuzitumia siku 12 zilizobaki kuiwinda Simba ambayo itakutana nayo. Kwanza walimsafirisha Lwandamina kwenda Ethiopia kuwatazama Dicha dhidi ya Makelakeya juzi Ijumaa, lakini alishindwa kuingia nchini humo baada ya kuzuiwa Uwanja wa Ndege wa Addis Ababa kutokana na hali ya usalama nchini humo. Lwandamina amerejea nchini jana mchana huku mabosi wa Yanga wakifanya mipango ya kumsafirisha leo alfajiri kumuwahisha Singida kuungana na kikosi chake.
Hata hivyo, bado Singida United wameshikilia ratiba ya Yanga katika kujiwinda na Simba, mchezo ambao utatoa taswira halisi ya ubingwa msimu huu. Kivipi? Kama Yanga itachomoza na ushindi dhidi ya Singida United hiyo leo na kutinga nusu fainali, itatibua mipango yote na kuilazimu kurudi fasta nyumbani kusubiri mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA, ambao umepangwa kupigwa katika ya Aprili 20 au 21.
Lakini, kama Yanga itaangukia pua kwa Singida United, basi mashabiki wafahamu mapema kuwa hawataiona timu yao na kwamba, itapiga kambi kule Ethiopia kumuwinda Mnyama.
MPANGO MZIMA
Wakati kikosi kikijiandaa na mchezo dhidi ya Singida, mabosi wa Yanga kupitia Kamati ya Utendaji waliitana kwa siri na kufanya majadiliano ya kina kuhakikisha msimu huu wanabeba mataji yote mawili ya ndani na kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mabosi hao chini ya uenyekiti wa Mhandisi Clement Sanga, pia waliijadili Simba na kupanga mkakati wa kuizima kwenye mechi yao hapo Aprili 29 ili kujiweka mahali pazuri kubeba ndoo kwa msimu wa nne mfululizo.
Katika kutimiza hayo, walikubaliana kuiweka timu kambini kule Ethiopia wakati watakapowafuata Dicha.
Lakini, kabla ya kikao hicho kizito, bosi wa Kamati ya Mashindano, Hussein Nyika walikutana na Lwandamina ili kupata ratiba nzima ya maandalizi ya mechi nne zinazofuata baada ya ile ya Singida United.
Baada ya kumalizana na Singida pale Namfua, nguvu zote zitaelekezwa kwa Dicha hapo Aprili 7, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya siku chache kuivuta tena Singida jijini Dar es Salaam kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara.
KAMBI ethiopia
Katika vikao hivyo, ratiba ya mechi za Yanga iliwekwa mezani na kuchambuliwa kwa kina, ambapo waliangalia mchezo unaofuata baada ya Singida United ni marudiano dhidi ya Wahabeshi kati ya Aprili 17-18 na kuamua kuibakisha timu huko huko Ethiopia.
Waliitazama ratiba na kubaini Yanga wakimalizana na Waethiopia hao mchezo unaofuata ni dhidi ya Simba, hivyo timu itaweka kambi ya muda nchini humo na wakitua hapa kazi ni moja kummaliza Mnyama.
“Tumekubaliana hizi mechi nne ni muhimu hivyo, tutumie nguvu kupata matokeo mazuri uwanjani. Tutakutana na Singida na baada ya hapo akili yetu itakuwa kwa hawa Waethiopia.
“Tunataka kutinga hatua ya makundi kwa kuwang’oa hawa Wahabeshi, tukimalizana kule kwao, timu itabaki huko na ikirudi ni siku mbili ama moja kabla ya kuikabili Simba. Hatutaki kelele za hapa nyumbani kwa sababu hawa jamaa zetu wanachonga sana.”
Chanzo: Mwanaspoti
MaoniMaoni Yako